Wanaume Kisumu waonywa dhidi ya kuwaambukiza Ukimwi wake zao wajawazito
IDARA ya Afya katika kaunti ya Kisumu imeelezea hofu kuhusu mwenendo wa wanaume kuwaambukiza virusi vya HIV wake zao waja wazito.
Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Fredrick Oluoch alisema kuwa wamegundua visa ambapo akina mama huwa hawana virusi hivyo miezi ya kwanza kabla ya kupata uja uzito lakini hupatikana na HIV wanapokaribia kujifungua.
Alisema hali hii huchangiwa na mwenendo wa wanaume kushiriki ngono na wapenzi wenye virusi hivyo kisha kuleta virusi hivyo kwa nyumbani kwa wake zao wenye uja uzito.
“Tunaendelea kushuhudia hali inayotishia ambapo mama hupimwa na kutopatikana na virusi miezi mitatu ya kwanza ya uja uzito na katika miezi tatu ya mwisho kabla ya wao kujifungua, hupatikana na virusi hivyo. Hii ina maana kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba walipata virusi hivyo kutoka kwa waume zao wanaoshiriki mapenzi bila kinga nje ya ndoa,” akasema Dkt Oluoch.
Afisa hiyo alisema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zilizofanyika katika Shule ya Msingi ya Kisian, Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi.
Haya yanajiri wakati Baraza la Kitaifa la Kudhubiti Magonjwa Sugu (NSCC) imetoa ripoti inayoonyesha kwamba Kisumu ni miongoni mwa kaunti zilizoandikisha viwango vya juu vya maambukizi mapya ya HIV nchini mnamo 2024.
Kiwango cha maambukizi ya HIV katika kaunti ya Kisumu ni asilimia 11 huku ikikadiriwa kuwa watu 111,367 wanaishi na virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.
Katika mwaka wa 2024, kaunti ya Kisumu iliandikisha maambukizi mapya 1, 341 ya virusi hivyo huku idadi ya wanawake ikiwa wengi (755) kuliko wanawake (361). Kwa upande mwingine, maambukizi mengine 225 yaliandikishwa katika watoto. Visa vya akina mama kuwaambukiza watoto wao (MTCT) vilipungua kutoka kima cha asilimia 9 mnamo 2019 hadi asilimia 5.97 mnamo 2024.
Dkt Oluoch alisema Idara ya Afya katika Kaunti ya Kisumu inaazimia kupunguza kiwango hicho cha maambukizi hadi chini ya asilimia tano (5).
Afisa huyo alisema japo visa vya maambukizi vimepungua kutokana na juhudi zinazoendeshwa kwa idara yake, juhudi hizo hata hivyo zinahujumiwa na mienendo ya wanaume kuwa na wapenzi wengi nje ya ndoa.
“ Wanaume hawa wanafaa kuwalinda wake zao waja wazito kwa kukoma kujihusisha katika ngono bila kinga na wapenzi nje ya ndoa. Wanapaswa kuwa watulivu, wawalinde wake zao nyakati za uja uzito,” akasema Dkt Oluoch.