HabariSiasa

Wandani wa Ruto waapa kupinga hoja za Serikali

February 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

IBRAHIM ORUKO na SAMWEL OWINO

WABUNGE wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wanapanga kupinga hoja na miswada ya Serikali itakayowasilishwa bungeni kulalamikia ‘kudunishwa’ kwake na waandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge hao pia wameapa kusambaratisha mipango yote inayowiana na muafaka wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bunge linarejelea vikao vyake Februari 12 baada ya likizo ya Krismasi iliyodumu kwa miezi miwili, huku shughuli nyingi zikiwa zinawasubiri.

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni Bajeti ya Ziada na miswada kadhaa muhimu ya serikali, ambayo inawiana na utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo, za Rais Kenyatta.

Miongoni mwa miswada inayosubiriwa kujadiliwa na kupitishwa ni ule wa Kawi, Uchimbaji Mafuta, Barabara, Unyunyiziaji Maji kati ya mingine. Mingi ya miswada hiyo iko katika Bunge la Seneti, na ndiyo iliyojadiliwa kwenye mkutano kati ya Rais Kenyatta na uongozi wa mabunge hayo mawili.

Wabunge hao wametishia kutopitisha Bajeti ya Ziada, kama ‘onyo’ kwa Rais Kenyatta kupunguza taharuki ya kisiasa iliyo katika chama cha Jubilee (JP).

Taharuki katika chama hicho imekuwa ikiongezeka tangu aliyekuwa naibu mwenyekiti wake, Bw David Murathe kusema chama hakitamuunga Dkt Ruto moja kwa moja kuwania urais ifikapo 2022.

Ghadhabu za kundi hilo zilizidi wiki iliyopita baada ya Rais Kenyatta kutangaza Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuwa Msimamizi Mkuu wa Miradi yote ya serikali. Wanamlaumu Rais Kenyatta kwa kumsaliti Dkt Ruto.