Wandani wa Ruto waingia baridi
Na WAANDISHI WETU
NAIBU Rais William Ruto anazidi kutorokwa na wandani wake ambao wanabadili misimamo yao na kufululiza hadi upande unaounga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Kwa muda mrefu, Dkt Ruto ameonekana kuchukua misimamo inayotofautiana na ile ya Rais Kenyatta hasa kuhusu suala la handisheki na utekelezaji wa ripoti ya jopo la maridhiano (BBI).
Vikao viwili vya hadhara vilivyofanywa kufikia sasa kuhamasisha umma kuhusu awamu ya pili ya BBI vilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa kikundi cha Tangatanga, huku duru zikisema kuna wengine wengi ambao watafuata mkondo huo hivi karibuni.
Mnamo Jumamosi katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Bw Odinga katika Kaunti ya Kakamega, wabunge Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Bernard Shinali (Ikolomani) walikuwa miongoni mwa wandani wa Dkt Ruto waliohudhuria.
Mkutano wa kwanza uliofanywa katika Kaunti ya Kisii pia ulihudhuriwa na baadhi ya wandani wa Naibu Rais wakiwemo Richard Tong’i (Nyaribari Chache), Prof Zadoc Ogutu (Bomachoge Borabu) na Marwa Kitayama (Kuria Mashariki).
Vilevile, wabunge Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba) na Oroo Oyioka (Bonchari) walitangaza wazi kukihama kikundi kinachoegemea upande wa Dkt Ruto.
Mbunge wa Naivasha, Bi Jayne Kihara ambaye pia ni mwandani wa Naibu Rais, alibadili msimamo wake mkali kuhusu BBI na badala yake akasema hatachukua msimamo wowote tena kwa sasa.
Alidai kwamba hali iliyoibuka kupitia kwa kampeni za kuhamasisha ripoti ya BBI zimeibua taharuki na watu wanachanganyikiwa kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
“Jinsi ilivyo kwa sasa, hatujui cha kutarajia kutokana na ripoti hiyo. Kibinafsi, nimeamua nisiegemee upande wowote kwa sasa,” akasema.
Katika eneo la Mlima Kenya, Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Bw Mpuru Aburi naye pia alikihama kikundi cha Tangatanga.
Bw Aburi ambaye amekuwa akimtetea sana Dkt Ruto alisema sasa ameamua kujiunga na kikundi kinachounga mkono mikutano ya hamasisho mashinani.
Alidai kuchukua hatua hiyo kwa kuwa Rais Kenyatta aliahidi kusuluhisha changamoto zinazokumba sekta ya kilimo.
Baadhi ya wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakilaumu maafisa wenye ushawishi katika serikali kuu kwa kutumia asasi za kiusalama kuhangaisha viongozi walio na misimamo tofauti na Rais Kenyatta.
Dkt Ruto akiwa katika Kaunti ya Machakos alilaani matukio yaliyoshuhudiwa Mumias ambapo wafuasi wake kutoka eneo la Magharibi walizimwa na polisi kufanya mkutano wao.
“Hakuna haja ya kuwakandamiza watu walio na misimamo tofauti hadi kuwanyima nafasi ya kujieleza,” akasema, huku akiungwa mkono na wanasiasa walioandamana naye.
Katika purukushani hizo za Mumias, Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali alitoweka katika hali tatanishi, hadi ikadaiwa alitekwa nyara.
Hata hivyo, mbunge huyo aliye pia kiranja wa wengi bungeni alijitokeza na kusema aliamua kutoroka baada ya maafisa wa polisi kuvamia nyumba yake Ijumaa usiku.
“Nilimwita rafiki yangu ambaye alinipeleka Kisumu nikakaa usiku kucha kisha nikaenda Nairobi asubuhi iliyofuata,” akasema jana.
Mbali na madai ya kukandamizwa na polisi, wafuasi wengine wa Tangatanga hudai kuwa serikali kuu inawafungulia kesi zisizo na msingi kortini ili kuwanyamazisha.
Ripoti za Shaban Makokha, Ruth Mbula, Macharia Mwangi, Charles Wanyoro na Valentine Obara