Wandani wa Ruto wataka wafafanuliwe maana ya demokrasia halisi
Na MWANGI MUIRURI na SAMMY WAWERU
VIONGOZI kutoka ngome ya kisiasa ya Rais Uhuru Kenyatta wanazidi kutoa hisia zao kuhusu ni ipi demokrasia halisi baada ya baadhi, hasa wanaojiegemeza katinga uungaji mkono wa azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais mwaka 2022, kudai wana habari kuwa idara za kiusalama zimeamrishwa ziwahangaishe.
Ndindi Nyoro ambaye ni Mbunge wa Kiharu amedai, “Kuna maafisa wakuu katika Wizara ya usalama wa ndani ambao wamepewa kazi ya kuwalenga wanasiasa wote walio nyuma ya uwaniaji wa Naibu Rais William Ruto katika kura ya 2022.”
Alisema kuwa yeye ni mmoja wa wale ambao wanalengwa na ndiyo sababu “sasa natangaza hadharani kwa Wakenya hasa wafuasi wangu katika Kaunti ndogo ya Kiharu wajiandae kupata njama hizo zikinilenga.”
Nyoro alisema kuwa ingawa anaheshimu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na chama cha Jubilee, ila akabainisha demokrasia halisi ni uhuru wa kujiamulia.
“Kuna wakereketwa wa udikteta ndani ya hii serikali ambao wanajitwika wajibu haramu wa kuamlia watu wataongea kuhusu lipi, waongee lini na waunge kauli gani mkono. Mimi ni mbunge wa Kiharu ambako mwasisi wa vita vya demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa, Kenneth Stanley Njindo Matiba alikuwa mbunge na pia mzawa,” akasema.
Alisema kuwa hatawahi kusaliti maono ya marehemu Matiba na kamwe hatafuata mkondo wa kushinikizwa bali atajiamulia mwenyewe akiwajibikia kauli za waliomchagua eneo la Kiharu.
Ni Kauli ambayo iliungwa mkono na mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi ambaye aliteta kuwa kuna njama za kuhangaisha wandani wa Ruto na tayari “tunajua watatumia Wizara ya Usalama wa Ndani ikiongozwa na Waziri Fred Matiang’i na katibu maalum, Karanja Kibicho.”
Alisema kuwa mamlaka ya ukusanyaji ushuru pia itajumuishwa huku vitengo vya kupambana na ufisadi vikipewa maagizo ya kuwaandama wandani wa Ruto.
Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alisema kuwa tayari yeye anahangaishwa na ndiyo sababu katika utawala wake kumejaa kelele za kila aina kuhusu uongozi mbaya, ufisadi na ukaidi.
“Nilitangaza haya mwishoni mwa mwaka 2018 lakini wengi hawakunielewa. Leo hii sasa mmeanza kushuhudia matukio ya kundi la watu katika afisi za hadhi na katika taasisi husika za kiusalama, harakati za kuhujumu demokrasia ya maamuzi, maongezi na ushirika,” akasema Waititu.
Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua aliteta kuwa “tayari hizo njama zilianza kushuhudiwa kitambo ambapo tulianza kuwaona baadhi ya maafisa wa kiusalama katika Kaunti wakikataa kujitokeza katika hafla za Ruto mashinani.
“Tunajua kuhusu njama hiyo… Tuko ngangari. Sio mara ya kwanza njama kama hizi zinazinduliwa. Zimekuwepo tangu Kenya ijipe uhuru wake wa kiutawala. Ingawa hivyo, cha kuridhisha na kututia moyo ni kuwa, hakuna hata wakati mmoja njama kama hizi zilifanikiwa. Hata kwa haya yetu ya Ruto, hakuna ufanisi utapatikana kwa hao wa kutuhujumu,” akasema Rigathi Gachagua.
Mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome aliteta kuwa kwa sasa ameanza kusukumiwa kesi za zamani ambazo zilikuwa zimefifia mahakamani.
“Waelewe kuwa wao ni maafisa wa kiusalama ambao wanawindana na wakili ambaye ni mimi. Nawaalika na sina wasiwasi nao. Lakini waelewe kuwa katiba inawazima kutekeleza miradi haramu na ikiwa hawajapokezwa maagizo hayo kupitia maandishi rasmi, wajue nitawaanika na niwageuze kitoweo kortini,” akasema Bi Wahome.
Aidha, Bi Wahome amekosoa matamshi ya Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, japo maoni ya mtu binafsi, kwamba Rais Uhuru Kenyatta anafaa hata kupewa fursa kupitia mabadiliko ya Katiba ahudumu kwa awamu nyingine baada ya 2022.
Mnamo Jumapili, Sonko alisema Rais Kenyatta anapaswa kuhudumu kwa awamu nyingine baada ya 2022 ili aweze kuafikia miradi ya maendeleo aliyoanzisha.
Bi Wahome amashikilia kwamba matamshi ya Sonko ni kauli yake binafsi ila si ya kiongozi wa taifa wala ya Jubilee.
“Hayo yalikuwa matamshi ya Sonko wala si ya Rais au chama cha Jubilee,” Bi Wahome akasema mnamo Jumanne.
Mbunge huyo na ambaye ni mmoja kundi linalounga mkono Ruto, alionya kwamba taifa likichukua mkondo wa matamshi ya aina hiyo huenda likagawanyika.
“Nchi haipaswi kuchukua mkondo huo. Hatutaki hali ambapo rais anatawala bila kuondoka madarakani,” alisema.
Mbunge huyo alisema viongozi waliochaguliwa wanapaswa kuwafanyia wananchi maendeleo kwa mujibu wa ahadi zao, ila si kuendesha siasa.
Wabunge wengine katika Jubilee wanaokosa matamshi ya gavana Sonko ni mwakilishi wa wanawake Kirinyaga Wangui Ngirici na mwenzake wa Laikipia Catherine Waruguru, mbunge wa Mukurweini Antony Kiai na Jayne Kihara wa Naivasha.
Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri naye alithubutu kusema sasa kuna utengano mkuu ndani ya serikali ya Jubilee, utengano unaoweza ukafanya vyama vilivyovunjwa ili kuunda chama cha umoja, kurejeshwa.
“Waelewe kuwa tuliamua. Na sisi sio watoto. Tuko tayari kupambana. Ikiwa wanajielewa, basi waandae kikao cha umoja na cha kuridhiana. Tuambiwe sisi kama Jubilee tunaelekea wapi na tunalenga nini 2022. Hili suala la kutulazimisha tujigeuze kuwa watumwa ndani ya siasa na vibarakala wa kungoja kuamuliwa ni mbinu za zamani na ambazo zimepitwa na wakati,” akasema Ngunjiri.