Habari

Wataenda wapi wahasiriwa wa mafuriko Januari?

December 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MAMIA ya Wakenya wangali wamepiga kambi katika shule mbalimbali nchini kufuatia mafuriko, huku shule zikiwa karibu kufunguliwa wiki ijayo.

Mafuriko na maporomoko ya ardhi yalikumba sehemu tofauti za nchi Desemba na kusababisha maafa mbali na uharibifu wa mali ikiwemo maboma.

Katika maeneo ya Nyanza, mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa wiki ilisababisha mafuriko mapya wakati ambapo waathiriwa wa awali wangali hawajapokea msaada wa kutosha kurejea makwao.

Katika Kaunti ya Homa Bay, kuna familia zilizohamia katika Shule ya Upili ya Odienya na Shule ya Msingi ya Nyarut zilizo Wadi ya Kochia, eneobunge la Rangwe, na Shule ya Msingi ya Bala iliyo eneobunge la Karachuonyo.

Familia hizo zimekuwa zikiishi hapo kwa zaidi ya wiki moja sasa.

Jumapili, viongozi mbalimbali wakiwemo Kamishna wa Kaunti David Kipkemei, Mbunge wa Rangwe Lilian Gogo na mwenzake wa Karachuonyo Adipo Kuome walitembelea waathiriwa hao kuwapelekea misaada ya muda.

Walitoa wito serikali kuu na ya kaunti kujitahidi kutoa suluhisho la kudumu kuhusu mafuriko kama vile ilivyofanywa Budalangi miaka iliyopita.

Kaunti ya Kisumu pia imekumbwa na mafuriko yanayolazimisha watu kuhama makwao hasa katika maeneo ya Nyando na Nyakach.

Hali kama hii inashuhudiwa katika kijiji cha Gachuha, eneobunge la Kipipiri, Kaunti ya Nyandarua ambapo familia kadhaa zilihamia Shule ya Msingi ya Gachucha.

Waliohama ni waathiriwa wa maporomoko ya ardhi yaliyotokea Ijumaa iliyopita.

“Maafisa wa serikali kuu walitutembelea Ijumaa jioni wakatushauri twende katika shule hiyo. Waliahidi kutuma misaada lakini kufika sasa hatujapokea. Watoto wetu wanateseka,” akasema mzee wa kijiji, Bw Samuel Kariuki.

Eneo jingine lililopata waathiriwa wengi wa maporomoko ya ardhi ni Kaunti ya Pokot Magharibi.

Katika Kaunti ya Kwale, ilani ilitolewa kuhusu mafuriko yanayotarajiwa kutokea upya huku waathiriwa wa awali wakiwa wangali wanatatizika.

Mafuriko hayo katika maeneo ya Vanga na Lunga Lunga husababishwa na mvua inayonyesha upande wa Tanzania.

Kaunti nyingine za Pwani ambazo ziliathirika sana na mafuriko ni Tana River na Taita Taveta.

 

Ripoti za Waikwa Maina, George Odiwuor, Fadhili Fredrick na Valentine Obara