Watambue wanachama 16 walioshiriki kuunda ripoti ya BBI
DICKENS WASONGA na VICTOR RABALLA
Jopo lililoandaa ripoti ya BBI lilijumuisha watu 14 na lilikuwa na makatibu wawili; Bw Paul Mwangi aliyewakilisha kinara wa ODM Raila Odinga na Balozi Martin Kimani aliyemwakilisha Rais Uhuru Kenyatta.
Balozi Dkt Martin Kimani (Katibu)
Ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kukabiliana na Mafunzo yenye Itikadi Kali (NCTC). Balozi Kimani ana digrii ya uzamifu (PhD) katika masuala ya kivita kutoka Chuo Kikuu cha King’s College kilichoko jijini London.
Amewahi kuwa balozi na mwakilishi wa Kenya katika Idara ya Mazingira (Unep), Makazi (UN Habitat) za Umoja wa Mataifa (UN).
Kwa kipindi cha miaka cha miaka 20 iliyopita, Dkt Kimani amefanya kazi katika masoko ya hisa ya kimataifa na mshauri wa usalama katika Upembe wa Afrika na Afrika Mashariki.
Paul Mwangi (Katibu)
Mnamo 2011, alikuwa mshauri wa Waziri Mkuu Raila Odinga kuhusu masuala ya Sheria na baadaye aliteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya sheria wa muungano wa NASA.
Alisomea digrii ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Bw Mwangi ni wakili ambaye amekuwa akiendesha kampuni yake ya kibinafsi.
Alikuwa mshauri mkuu wa upande wa ‘HAPANA’ ulioshinda kura ya maamuzi mnamo 2005.
Yusuf Haji (Mwenyekiti)
Ni mwenyekiti wa jopo la BBI alizaliwa mnamo 1940 wilayani Garissa. Anatoka katika ukoo wa Ogaden Dorad. Haji alisomea masuala ya usimamizi na udhibiti wa fedha kiwango cha diploma katika Chuo Kikuu cha Birmingham.
Aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Wilaya na Mkoa kati ya 1970 na 1997. Mnamo 1998 aliteuliwa kuwa mbunge maalumu na baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Ijara.
Wakati huo alihudumu kama naibu waziri katika afisi ya Rais.
Amos Wako
Amos Wako alizaliwa mnamo 1946 wilayani Busia. Ni wakili na aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Sheria kwa kipindi cha miaka 20 chini ya utawala wa Rais Daniel Arap Moi.
Alikuwa Mkuu wa Sheria wa nne kati ya 1991 na 2011. Bw Wako sasa ni Seneta wa Busia kupitia tiketi ya chama cha ODM.
Alisomea katika shule ya Upili ya Kakamega na Alliance na kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha London ambapo alisomea Sayansi ya Masuala ya Uchumi.
Baadaye alisomea digrii ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alisomea Sheria kiwango cha Uzamili katika Chuo Kikuu cha London.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Sheria, alihudumu katika taasisi na mashirika mbalimbali yanayohusiana na sheria.
Aliandika sheria mbalimbali za kufanyia mabadiliko Katiba, ikiwemo sheria ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi na kubuniwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.
Kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali, Wako aliongoza kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba mpya iliyojulikana kama ‘Wako Draft’.
Rasimu hiyo, hata hivyo, ilikataliwa na Wakenya wakati wa kura ya maamuzi ya 2005.
Rais Moi alipong’atuka kutoka uongozini mnamo 2002, Wako aliendelea kuhudumu kama Mkuu wa Sheria wakati wa utawala wa Mwai Kibaki.
Agnes Kavindu
Aligonga vichwa vya habari alipopewa tiketi ya chama cha Jubilee kuwania kiti cha Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Machakos.
Kavindu, 60, alikuwa mke wa aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnston Muthama.
Ni mhubiri ambaye hujulikana kama Pasta Agnes. Anahubiri katika Kanisa la Kyemutheke A.I.C katika eneo la Maua, Machakos.
Zacchaeus Okoth
Askofu Mkuu Zacchaeus Okoth wa parokia kuu ya Kisumu alizaliwa mnamo Julai 5, 1942 katika eneo la Nyakach, Kaunti ya Kisumu.
Alitawazwa kuwa askofu mnamo Novemba 14, 1968 na aliteuliwa kuwa askofu wa Kisumu mnamo 1978.Aliteuliwa kuwa askofu wa parokia kuu ya Kisumu mnamo Mei 1990 na alistaafu Novemba 15 mwaka huu.
Katika kitabu chake: An Enigma in Kenyan Politics, Bw Odinga anasema kuwa Askofu Mkuu Okoth alimsaidia pakubwa kukwepa mtego wa serikali wakati wa harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi.
Baada ya kupokea ripoti kutoka kwa ubalozi wa Amerika kwamba serikali ya Moi ilipanga kumkamata, Bw Odinga alitoroka Kenya kupitia Rang’ala ambapo alilala akijifanya kuwa askofu wa Kanisa Katoliki kwa msaada wa Okoth.
Baadaye alitorokea Uganda kupitia Ziwa Victoria kupitia ufukwe wa Olago.
Dkt Adams Oloo
Alizaliwa mnamo 1967 wilayani Siaya. Ni mhadhiri mkuu wa masuala ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Ni mkuu wa Kitivo cha Elimu ya Sayansi wadhifa ambao wamekuwa akishikilia tangu 2011.
Alisomea Sayansi ya Siasa kiwango cha uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Delaware, Amerika.Hufunza kozi mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Nairobi na Delaware.
Meja John Seii
Ni jenerali wa zamani wa jeshi aliyetoka jeshini mnamo 1983 kutokana na anachosema alifutwa kazi kwa kuonewa na utawala wa Moi.
Anasema masaibu yake yalisababishwa na aliyekuwa waziri mwenye nguvu, marehemu Nicholas Biwott.
Seii aliwania kiti cha ubunge mnamo 1992 na 1997 lakini akabwagwa na Nicholas Biwott.
Kulingana na mkewe, Tabitha Seii, Meja (Mstaafu) Seii alitimuliwa jeshini baada ya kuitaka serikali kuruhusu mfumo wa vyama vingi kwa kufutilia mbali kifungu cha 2A cha Katiba kilichopiga marufuku vyama vingine mbali na Kanu.
Amekuwa akifanya shughuli mbalimbali za kurejesha amani katika eneo la Bonde la Ufa, haswa baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007.
Kwa sasa, Seii ni Mwenyekiti wa Baraza la jamii ya Wakalenjin Myoot na mwenyekiti wa Vuguvugu la Kutetea Amani Uasin Gishu.Katika uchaguzi uliopita wa 2017, anakumbukwa kwa kutoa pendekezo kwamba viti vya uongozi katika Kaunti ya Uasin Gishu vigawanye kwa kila jamii.
Pendekezo hilo lilionekana kumpendelea Gavana Mandago aliyekuwa akikabiliwa na upinzani kutoka kwa bwanyenye Zedekiah Bundotich, maarufu Buzeki.
Askofu Peter Njenga
Ni askofu mstaafu wa Parokia ya Mt Kenya ACK na sasa ni mwenyekiti wa jamii za Gema (Chama cha Wakikuyu, Waembu na Wameru).
Amekuwa katika mstari wa mbele katika kupigania amani na usawa.
Rose Museo
Rose Museo ni Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Makueni na alikuwa mjumbe wa jopo la chama cha ODM lililokuwa likitatua malalamishi ya wawaniaji walioshiriki kura za mchujo kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Bi Museo alianzisha vuguvugu la wanawake linalofahamika kama Ukambani Women Network (UKAWONE) lenye wanachama 98 ambao wanakopeshana hela na kujihusisha katika shughuli za kuteka maji ya mvua na uhifadhi wa mazingira.
Alianzisha vyama vya kuwezesha wanawake kuwekeza fedha katika ukanda wa Pwani ambapo kuna jumla ya wanachama 498 waliojiunga na makundi; Saveten Women of Pwani na Kobole Sisters.
Maison Leshomo
Ni Mwakilishi wa Kike wa Wanawake wa Kaunti ya Samburu kupitia tiketi ya chama cha Kanu.Amewahi kuwa mbunge Maalum na mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake tawi la Samburu.
Saeed Mwaguni
Ni profesa wa Sayansi ya Mazingira katika Chuo Kikuu cha Technical, Mombasa.Hujihusisha na masuala ya Sera na Mipango.
Amewahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Ustawi wa eneo la Pwani na Maabara Kuu ya Serikali.
Dkt Morompi ole Ronkei
Amewahi kuhudumu kwa miaka mingi katika rubaa za kimataifa ambapo alishikilia nyadhifa mbalimbali.
Dkt Ronkei ana shahada ya Uzamifu ( PhD) katika uanahabari ambayo aliipata katika Chuo Kikuu cha Oregon, Amerika.
Amewahi kuifanyia kazi Benki ya Dunia na hata kufanyia utafiti serikali za Kenya, Tanzania na Ghana.
James Matundura
Mzee James Matundura ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta na ni mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Wakisii.
Matundura anawakilisha jamii ya Wakisii katika kikosi cha kushauri rais.Alizaliwa kijijini Ivacho, Kisii mnamo 1948.
Alisomea katika shule ya Msingi ya Ivacho na baadaye akajiunga na shule ya Upili ya Gesusu.Alihudumu kama chifu kati ya 1985 na 2002.
Amewahi kutunukiwa na Rais Kenyatta na Mwai Kibaki kwa kuongoza juhudi za amani katika maeneo ya Kisii.
Askofu Lawi Imathiu
Kasisi Imathiu alizaliwa mnamo 1932 kijijini Kaaga. Mnamo 1950, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Meru ambapo alihitimu 1952 na kuwa mwalimu.
Baadaye alijiunga na Chuo cha Theolojia cha St Paul’s mnamo 1954 na kisha Chuo cha Theolojia cha Epiworth nchini Zimbambwe mnamo 1958.
Baada ya kuhudumu kama mhubiri wa Kanisa la Methodist kwa miaka mitatu, alijiunga na Chuo cha Theolojia cha Lincoln, uingereza na baadaye Chuo Kikuu cha London.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Elimu ya Kidini cha Claremont, Amerika ambapo alihitimu shahada ya uzamili mnamo 1983.
Florence Omose
Ni mwandani wa chama cha ODM na aliwahi kuhudumu katika jopo la kutatua mizozo la chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.