Watatiza nchi kwa siasa za ubabe
Na WANDERI KAMAU
MZOZO wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto umegeuka kero kwa maendeleo, umoja na usalama wa nchi.
Wachanganuzi wanaeleza kwa Rais na Naibu Rais kukosa kushirikiana, utendakazi serikalini unatatizika, na wanaoumia ni wananchi, huku wafuasi wao wakizuia ghasia na kurushiana matusi na chuki mitandaoni.
Kwa mujibu wa Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa, ushindani wa kisiasa unaoshuhudiwa kwa sasa unatokana na tamaa ya viongozi husika na ubinafsi.
Anasema mwelekeo huo unajenga hali ambapo ni vigumu hali ya kuaminiana kuwepo katika siasa nchini, ambapo matokeo yake yamekuwa ni wananchi kukosa kuhudumiwa ipasavyo na uadui baina ya raia.
Mnamo Jumapili watu wawili waliuawa katika Kaunti ya Murang’a kwenye ghasia kati ya wafuasi wa Rais Kenyatta na wale wa Dkt Ruto.
“Tamaa na maslahi ya kibinafsi ndiyo misukumo halisi inayowafanya viongozi kuungana kisiasa. Hawajali uwepo wa malengo au mikakati ya muda mrefu itakayowafaidi wananchi bali wao wenyewe kibinafsi. Ukosefu wa malengo yaliyokitwa kwenye ustawi wa kisiasa daima utatufanya kukwama kama nchi ikiwa hili halitarekebishwa,” akasema.
“Hali ya mikataba kubuniwa na kuvunjika ni jambo la kawaida kwenye siasa kwani lengo kuu la wahusika huwa ni kuona ikiwa watatimiza maslahi yao,” asema mtaalamu wa siasa Prof Macharia Munene.
Wafuasi wa Dkt Ruto na Rais Kenyatta wamekuwa wakilaumiana kila upande ukidai kusalitiwa na mwingine.
Upande wa Naibu Rais unasisitiza kuwa Rais Kenyatta amemsaliti naibu wake kwa kwa kutozingatia ahadi ya kumuunga mkono kuwania urais wa 2022, licha yake kuahidi wakati wa kampeni.
Mrengo wa Rais Kenyatta nao unasema Dkt Ruto ndiye wa kulaumiwa kwa kuanza kampeni za mapema kinyume na ushauri wa Rais.
Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta anasema Dkt Ruto ndiye aliyeanza kuyumbisha jahazi la Jubilee alipoanza kampeni za mapema za 2022.
“Hatua ya Dkt Ruto kuanza kampeni mapema ni kumchokoza Rais moja kwa moja. Ni vipi mume anaweza kukaa na mke ambaye hamheshimu?” akasema Bw Murathe.
Lakini Bw Murkomen anamkosoa Rais Kenyatta akisema ndiye chanzo kikuu cha mtafaruku uliopo kati yake na Dkt Ruto na pia ndani ya Jubilee.
“Jubilee imegeuka kuwa nyumba inayoongozwa na mtu mmoja ambaye usemi wake ndio amri. Hivyo ndivyo chama kinapaswa kuongozwa?” anashangaa Bw Murkomen, ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto.
Kwa mujibu wa Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mdadisi wa siasa, si mshangao mzozo wa sasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, kwani msingi wa muungano wao ulijengwa kwenye mashtaka yaliyowakabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mnamo 2012.
“Muungano wa UhuRuto uliwahusisha waathiriwa wawili wa mchakato wa ICC, wala si marafiki wa kweli. Ilitegemewa ungesambaratika mara tu baada ya mashtaka yao kukamilika,” aeleza Prof Kagwanja.
Aliongeza kuwa katika kubuni Jubilee, wawili hao walikosa kutatua changamoto za kisiasa zilizochangia ghasia za kikabila za 2007/2008.
Anaonya kuwa mtindo wa miungano kuvunjika kila mara ni ishara kuwa huenda Kenya ikachukua muda mrefu kupatauthabiti wa kisiasa.
Bw Bigambo anasema tabia hii ya usaliti katika siasa ina madhara zaidi kwa wananchi hata kuliko wanasiasa wahusika: “Ikiwa wanasiasa wanaweza kusalitiana baina yao, je, ni kiasi kipi wanaweza kuwasaliti wananchi waliowachagua?”