Habari

Watermelon mpya?

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto jana Jumanne aliendelea kuonyesha kutokuwa na msimamo kuhusu Mswada wa marekebisho ya Katiba, BBI, na kuibua maswali miongoni mwa Wakenya kama yeye ndiye ‘Watemelon’ mpya.

Akizungumza Jumanne akiwa Kaunti ya Nakuru kwenye mazishi ya mamake mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, Dkt Ruto alisisitiza kuwa hana nia ya kupinga mageuzi yaliyopendekezwa kufanyiwa katiba, bali anachotaka ni maoni ya kila mtu kushirikishwa.

“Tunaweza kutafuta uwiano na makubaliano badala ya kuzua uadui kwa kusukuma watu kuwa katika mirengo hii au ile,” alisema.

Kutokueleweka upande anaosimama kumewafanya baadhi ya makundi ya kisiasa yamsukume, jambo analosema hataliruhusu, kwa kuwa akifanya hivyo ataonekana mbaya machoni pa Wakenya.

Akionekana kumlenga kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga ambaye amekuwa akimlaumu kwa msimamo wake kuhusu mchakato huo, Dkt Ruto alisema enzi za Wakenya kuishi kama maadui zimepita na ana hakika BBI haitawagawanya Wakenya.

“Tusisukume mtu eti kwa sababu ana maoni tofauti awe adui, tukamwambia wewe hufai. Tunafaa kuungana tusonge mbele kama watu wa taifa moja,” Dkt Ruto alisema.

Bw Odinga amekuwa akipuuza wito wa Dkt Ruto kwamba ripoti ya mwisho ya BBI ibadilishwe ili kushirikisha maoni ya makundi na watu waliolalamika.

Dkt Ruto hakuhudhuria hafla ya kuzindua ukusanyaji wa saini za kuunga mswada utakaowasilishwa katika kura ya maamuzi kufanyia katiba marekebisho.

Ingawa ukusanyaji wa saini unaendelea kuunga mswada wa BBI, Dkt Ruto alisisitiza kuwa ana imani kuwa mchakato huo hautawafanya Wakenya kugawanyika.

“Tunataka kujenga uwiano ili tusonge mbele kama Wakenya. Inawezekana na nina imani itawezekana,” alisema.

Alisema kuwa lengo la wasiotaka makubaliano kuhusu mpango huo wanataka Wakenya wagawanyike.

Kwa mara ya kwanza na bila kufafanua, Dkt Ruto alikiri kwamba amekuwa na tofauti Kati yake na Rais Kenyatta lakini akasema huo haimaanishi kuna tatizo Kenya.

“Sio kwamba eti mimi na Rais Kenyatta hatuna tofauti lakini kuna mengi yanayotuunganisha kuliko kututenganisha,” alisema.

Uhusiano wa wawili hao umekuwa baridi tangu mchakato wa kubadilisha katiba ulipoasisiwa miaka miwili iliyopita kufuatia handisheki ya Rais Kenyatta na Bw Odinga. Wakati wa kuzindua ripoti BBI, Rais Kenyatta alimlaumu Dkt Ruto kwa kukosoa baadhi ya mapendekezo.

Wiki jana, Dkt Ruto alikosa kuhudhuria mkutano muhimu wa Baraza la Taifa la Usalama (NSC) uliofanyika katika kambi moja ya kijeshi kaunti ya Samburu. Mkutano huo ulipokuwa ukiendelea, Dkt Ruto alikuwa akikutana na wandani wake kujadili hatua msimamo watakaochukua kuhusu BBI.

Naibu Rais alisema hatakubali kiongozi yeyote kuchochea ghasia za kikabila eneo la Rift Valley na akawataka wakazi kutowachagua viongozi wanaowatenganisha.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, alitunukiwa lakabu ya Watermelon na wanasiasa wanaomuunga mkono Kinara wa ODM, Raila Odinga wakati wa marekebisho ya kwanza ya katiba ya 2010 kutokana na kile walichodai kuwa kutokuwa na msimamo kuhusu mageuzi hayo.