Watu 26 waangamia baada ya shambulizi katika hoteli maarufu Kismayo
Na AFP
MOGADISHU, SOMALIA
WATU si chini ya 26 wakiwemo raia wa kigeni kadhaa, wameuawa huku 56 wakipata majeraha katika shambulizi la bomu la kujitoa mhanga katika hoteli maarufu Kusini mwa Somalia, amesema afisa wa kieneo mapema Jumamosi.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekiri kuhusika.
Mhanga aliyetekeleza shambulizi hilo alifululiza gari lenye vilipuzi katika hoteli ya Medina katika bandari ya Kismayo mnamo Ijumaa muda mchache kabla ya watu kadhaa waliokuwa wamejihami kwa bunduki kuingia katika hoteli hiyo huku wakimimina risasi kiholela, maafisa wamesema.
Shambulizi hilo lilichukua takribani saa 12 ambapo limefika kikomo Jumamosi baada ya maafisa kukabiliana na magaidi hao.
Wakenya watatu, ikiwa ni idadi sawa ya Watanzania, raia wawili wa Amerika, raia mmoja wa Uingereza na mmoja wa Canada ni miongoni mwa watu 26 walioangamia, kulingana na taarifa ya Rais Ahmed Mohamed Islam wa Jubaland – eneo ambalo kwa kiasi fulani linajitawala – ameambia vyombo
“Pia kulikuwa na raia wawili wa China waliopata majeraha,” amesema Ahmed Mohamed.