Habari

Watu wanane wafariki katika mkasa wa moto mtaani Kibra

Na NDUBI MOTURI May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATU wanane walifariki dunia na wengine saba kulazwa hospitalini baada moto kuteketeza zaidi ya nyumba 70 za mabati katika mtaa wa Kibra, Nairobi, Jumamosi alfajiri.

Moto huo ulizuka mwendo wa saa kumi na moja asubuhi na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wakazi waliokuwa wamelala. Kwa baadhi ya waathiriwa, kama Bi Nafisa Burhan, taharuki ilianza baada ya kusikia milio ya pikipiki na mayowe ya wanawake waliokuwa wakihangaika kujiokoa.

“Nilidhani ni kelele za mama mboga waliokuwa wamevamiwa, lakini nilipofungua mlango, niliona moshi mzito na moto ukiwaka. Niliona wanawake wakikimbia, mmoja wao akarudi kuchukua mwanawe aliyekuwa amelala, lakini hakufanikiwa kutoka,” alisema Bi Burhan kwa majonzi.

Wakazi walijaribu kuzima moto kwa kutumia maji , lakini juhudi hizo hazikufaulu kwa kuwa ulienea kwa kasi.

“Tulisikia mayowe ya watu waliokuwa wamekwama ndani, lakini baadaye yakatulia. Hatukuwa na uwezo wa kuwaokoa,” alisema kwa huzuni.

Moto huo ulidhibitiwa saa moja asubuhi kwa msaada wa idara ya zimamoto ya Kaunti ya Nairobi. Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Maafa, Bw Bramwel Simiyu, alithibitisha kuwa nyumba 71 zilichomeka na familia kadhaa kuachwa bila makazi.

“Tulisaidiana na jamii kuuzima moto. Tumewapeleka majeruhi hospitalini, ingawa kwa masikitiko tumepoteza maisha ya wakazi nane,” alisema Bw Simiyu.

Kamanda wa Polisi wa Nairobi, George Seda, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda moto huo ulisababishwa na uunganishaji haramu wa umeme au mshumaa uliosahaulika.

“Bado tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo  halisi cha moto huo,” alisema Bw Seda.

Mmoja wa walioshuhuda, Bw Abdul Karim, alisimulia tukio la mama mjamzito aliyefariki akiwa katika harakati za kujiokoa.

“Alikuwa anakimbia kutoka ndani ya nyumba lakini moto ulimzidi. Nilijaribu kumuokoa lakini sikuweza,” alisema kwa masikitiko.

Wakazi sasa wanatoa wito kwa serikali kuwasaidia waathiriwa wa mkasa huo na kuchukua hatua kuhakikisha usalama katika mitaa ya mabanda