Wetang'ula asema sakata ya dhahabu ni suala dogo kwake
Na LEONARD ONYANGO
KIONGOZI wa Ford Kenya Moses Wetang’ula amekanusha madai kwamba amealikwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuenda kuandikisha taarifa kuhusu sakata ya dhahabu feki.
Bw Wetang’ula Jumatano alisema hajapokea mwaliko wowote kutoka kwa DCI kuhusiana na sakata ya dhahbu feki.
“Sakata hiyo hainishtui mimi,” akasema Bw Wetang’ula alipokuwa akihutubia wanahabari katika makao makuu ya Ford Kenya, Nairobi.
“Mimi nilikuwa na mkutano na viongozi wa chama cha Ford Kenya na nikitoka hapa naenda kufariji familia ya aliyekuwa mbunge wa Amagoro Fredrick Oduya Oprong,” akasema Seneta wa Bungoma.
Oprong aliaga dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 83.
Awali, kulikuwa na madai kwamba Bw Wetangula alitarajiwa mapema Jumatano kufika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusiana na sakata ya dhahabu bandia.
Wiki iliyopita, Idara ya DCI ilisema kuwa tayari imeharifiwa kuhusiana na sakata hiyo na tayari imeanzisha uchunguzi ili kuwanasa waliotekeleza ulaghai huo.
Sauti
Bw Wetang’ula amejipata pabaya baada ya kanda ya sauti kuchipuza katika mitandao ya kijamii ambapo amesikika akizungumza na mfanyabiashara kutoka Dubai kuhusu shehena ya dhahabu inayodaiwa kuzuiliwa na serikali katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Katika kanda hiyo Bw Wetang’ula anasikika akiahidi kuzungumza na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ili shehena hiyo iachiliwe.
Sakata hiyo ya dhahabu bandia imemfaa kisiasa Naibu wa Rais William Ruto, ambaye sasa anawakashifu vigogo wa NASA kwa masaibu ya kulaghaiwa ufalme wa Dubai.
Dkt Ruto alilaumu upinzani kuwa umekuwa ukijifanya kuwa safi, ilhali kichinichini unaendesha mambo ya ukora.
“Upinzani ulilaumu Jubilee kuwa iliiba Eurobond na kuwa tumeuza Bandari ya Mombasa, ambao ulikuwa uongo. Sasa wanauza dhahabu feki. Wakenya sasa wanajua wakora ni kina nani,” akasema.
“Viongozi wengine waache kujifanya kuwa watakatifu ilhali hao ni sehemu ya wale wanaohusika na biashara za vitu feki kama hiki kisa cha dhahabu,” akasema.