Habari

Wito uwanja wa Talanta ubadilishwe jina kumuenzi Hayati Raila Odinga

Na WINNIE ONYANDO December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja ametoa wito kwa serikali ya Rais William Ruto kubadilisha jina la uwanja wa Talanta kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.

Gavana huyo alitoa wito huo wakati wa sherehe za 62 za Jamhuri katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi.

Gavana Sakaja alitumia hotuba yake kumrai rais kuzingatia maombi ya wakazi wa Nairobi wanaotaka uwanja huo upewe jina Raila.

Matamshi yake yalipokelewa kwa shangwe kwani hii ndio Jamhuri Dei ya kwanza kusherehekewa bila Raila kuwepo.

Sakaja aliambia umati kuwa kuanzia mwaka ujao, hafla kuu za kitaifa zitaandaliwa katika uwanja wa Talanta, akiongeza kuwa wakazi wa Nairobi waliona inafaa kukipa kituo hicho jina la Raila Amolo Odinga Stadium, ombi lililoibua shangwe kutoka kwa waliohudhuria sherehe hizo.

“Tunajua kuwa kuanzia mwaka ujao, zoezi hili litafanyika katika uwanja wa Talanta hapa Nairobi. Kwa niaba ya wakazi wa Nairobi, tunakuomba ukubali kubadilisha jina la uwanja huo kuwa Uwanja wa Kimataifa wa Raila Amolo Odinga, kama njia ya kutoa heshima kwa Bw Odinga,” Sakaja alisema.