Habari

Wito wanaume watafute ushauri nasaha visa vya kitanzi vikizidi Mpeketoni

Na KALUME KAZUNGU January 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WANAUME katika Kaunti ya Lamu wamehimizwa kutafuta ushauri nasaha badala ya kujitoa uhai wanapokumbwa na changamoto za kimaisha.

Kulingana na ripoti za polisi, visa vya wanaume kujinyonga, hasa tarafa ya Mpeketoni, Lamu Magharibi vimeongezeka siku za hivi punde.
Wanaume wasiopungua 10 wamejitoa uhai katika kipindi cha mwezi mmoja.

“Visa vya watu, hasa wanaume kujinyonga vimezidi. Ninawahimiza watu wasinyamaze. Badala ya kujitoa uhai, tafuta ushauri nasaha unapobanwa na jambo lolote,” akasema Naibu Kamishna wa Lamu Magharibi Gabriel Kioni.

Maeneo yaliyoshuhudia visa hivyo ni Nairobi Area, Mapenya, Sina Mbio, Bomani, Hongwe, Umoja, Mpeketoni Mjini, Baharini, Hindi Mjini na viunga vyake.

Bw Kioni alisema idara ya polisi ina kitengo maalum cha kushughulikia ushauri nasaha, akiwasihi wananchi kutumia huduma hizo kujiokoa.
Wanaume sasa wanashinikiza kuanzishwa kwa kituo cha ushauri nasaha kuepuka visa vya kujitoa uhai.