Yaelewe mabadiliko katika ripoti ya BBI na mswada wake
Na CHARLES WASONGA
KAMATI ya kiufundi ya mchakato wa maridhiano (BBI) imefanya mabadiliko kadha katika ripoti na mswada wa awali uliozinduliwa mnamo Oktoba 26, 2020, katika ukumbi wa Bomas.
Hii ni licha ya kwamba kiongozi wa ODM Raila Odinga amekuwa akisisitiza kuwa ripoti hiyo ya BBI haitafanyiwa marekebisho mengine.
Miongoni mwa mabadiliko makuu ni kubuniwa kwa wadhifa wa Naibu Mawaziri ambao pia wanaweza kuteuliwa kutoka bungeni.
Katika mswada wa awali, nyadhifa hizo hazikuwepo japo pendekezo la kuteuliwa kwa baadhi ya mawaziri kutoka bungeni lilikuwepo.
Ripoti ya sasa pia imedumisha pendekezo la uteuzi wa baadhi ya mawaziri kutoka bungeni “ili kurahisisha utendakazi wa wabunge.”
Mswada wa sasa pia unawaruhusu Magavana kuteua baadhi ya mawaziri wao kutoka miongoni mwa madiwani. Pendekezo hili lilikuwa limetolewa na Muungano wa Mabunge ya Kaunti (CAF).
Vile vile, mswada wa sasa umeondoa pendekezo la kubuniwa kwa Baraza la Polisi Nchini (KPC) ili kuchukua nafasi ya Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC). NPC ingesimamiwa na Waziri wa Masuala ya Ndani.
Kuhusu uteuzi wa afisa wa kupokea malalamishi kutoka kwa majaji (Judiciary Ombudsman), uteuzi wake sasa sharti uidhinishwe na Bunge la Seneti, kulingana na mswada huu mpya.
Pendekezo la kuhamishwa kwa majukumu manne makuu kutoka Serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu pia limeondolewa.
Idadi ya maene bunge imeongezwa kutoka 290 hadi 360 kupitia pendekezo la kubuniwa kwa maeneobunge mapya 70. Nao wabunge sita watateuliwa kuwakilisha makundi ya walemavu na vijana; wanne watawakilisha walemavu na wawili watawakilisha vijana.
Katika bunge la Seneti, mswada huu mpya wa BBI unapendekeza kuwa jumba hilo liwe na wajumbe 94. Hii ina maana kuwa kila moja ya kaunti 47 zitachagua maseneta wawili; mwanamume mmoja na mwanamke mmoja.
“Na endapo usawa wa kijinsia hautafikiwa baada ya uchaguzi mkuu, wabunge zaidi watateuliwa jinsi inavyofanyika katika mabunge ya kaunti,” mswada huo unasema.
Hii ina maana idadi kamili ya wajumbe katika bunge la kitaifa huenda ikazidi 366; hadi pale hakuna jinsia ambayo itakuwa na uwakilisha wa zaidi ya thuluthi mbili ilivyo wakati huu.
Wabunge 70 zaidi wanaopendekezwa watatoka katika kaunti ambazo zina idadi kubwa ya watu na ambazo wakazi wanahisi kuwa hawajawakilishwa ipasavyo.
Hii ndio maana Kamati ya Kiufundi ya BBI imependekeza kuwa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ichore upya mipaka ya maeneo bunge baada ya kufanyika kwa kura ya maamuzi.
Kaunti ambazo wakati zina uwakilishi mdogo wa wabunge kwa sababu ya kuwa na idadi kubwa ya watu ndizo zitaongezewa idadi ya maeneo bunge. Kisheria, kila eneo bunge linapasa kuwa na watu 132,138.
Baadhi ya kaunti ambazo zitaongezewa maeneo bunge kwa misingi hiyo ni Nairobi ambayo itapata maeneo bunge 12 zaidi Kiambu (6), Nakuru (5), Kilifi (4), Mombasa (3), Bungoma (3) na Kajiado inaongezewa maeneobunge matatu (3).
Kaunti ya Nairobi itasalia kuwa huru baada ya pendekezo la kuiweka Idara ya Huduma za Jiji (NMS) ndani ya Katiba.
Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akishiniza kuwa Serikali ya Kitaifa itwae kabisa majukumu makuu ya Kaunti ya Nairobi, kupitia marekebisho ya katiba inayopendekezwa na BBI.
Kulingana na ripoti ya BBI iliyozinduliwa mnamo Oktoba 26, 2020, majukumu ya kaunti ya Nairobi kama vile Afya, Uchukuzi, Mipango, Ujenzi, Idara ya Zimamoto na Usimamizi wa Majanga zihamishwe hadi Serikali ya Kitaifa.
Hii ingetekelezwa kupitia marekebisho ya Mpangilio wa Nne, unaoorodhesha mamlaka na majukumu ya serikali za kaunti.
“Sheria itabuniwa ya kufafanua kuhusu majukumu ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi na yale ya Serikali ya Kitaifa chini ya Mpangilio ya Nne,” ripoti ya BBI iliyozinduliwa Oktoba 26, 2020, ilisema.
Mabadiliko mengine kwenye mswada wa sasa wa BBI ni kwamba vyama vya kisiasa havitakuwa na wajibu wowote katika uteuzi wa Makamishna wa IEBC.
Mswada huo unapendekeza kuondolewa kwa makamishna wa sasa wa tume hiyo na kuteuliwa kwa wapya kama “hatua ya kuimarisha uwezi wa tume hiyo kuendesha uchaguzi huru na wa haki.