Yafichuka ODM ilipanga kuiba kura 2007
Na MWANDISHI WETU
SHIRIKA la kimataifa linalosifika kwa ufichuzi wa maovu ya kiuongozi, limetoa nakala ya siri ya Chama cha ODM inayoonyesha kilipanga kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2007.
Kulingana na nakala hiyo iliyofichuliwa Jumapili na shirika la Wikileaks, imesemekana wizi wa kura ulikuwa miongoni mwa mikakati michafu ya kisiasa ambayo ODM iliweka katika juhudi za kujaribu kuhakikisha kiongozi wa chama Raila Odinga angeibuka mshindi.
Katika uchaguzi huo tatanishi, Rais Mstaafu Mwai Kibaki ndiye alitangazwa mshindi, hali iliyosababisha ghasia ambazo zilipelekea watu zaidi ya 1,000 kuuliwa na maelfu wengine kufurushwa makwao.
Wakenya sita, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kudaiwa kuhusika kupanga ghasia hizo.
“Tutahakikisha watu hawafuatilii mienendo yetu ili endapo tutapata mwanya, tutautumia kujiongezea kura katika ngome zetu,” inasema sehemu ya nakala hiyo.
Kando na wizi wa kura, nakala hiyo ya siri katika ODM imeonyesha kuwa chama hicho kilikusudia kuzua taharuki na ghasia endapo mipango yote ya kumfikisha Bw Odinga katika Ikulu haingezaa matunda.
Kwa mujibu wa nakala hiyo, mpango huu wa ghasia ungefanikishwa kwa kutumia maajenti wa ODM mashinani kuzua uhasama, kutoa misaada kwa makundi ya kivita Mlima Elgon na kusambaza karatasi zenye jumbe za chuki ya kikabila maeneo mbalimbali.
Jukumu hili lilitwikwa mmoja wa wanajeshi wastaafu wa daraja la juu aliyehudumu katika serikali ya mmojawapo wa rais wastaafu nchini.
Imesemekana siasa chafu za ODM hazikuishia hapo, kwani kulikuwa na mpango wa kusudi kufanya jamii mojawapo kubwa nchini ionekane kama ya waovu ili jamii nyingine zote kitaifa ziungane kumchagua Bw Odinga.
ODM pia imedaiwa ilipanga kuchochea wakazi wa maeneo wanaotamani utawala wa Majimbo dhidi ya serikali kuu kama vile Rift Valley, Magharibi na Pwani.
Ili kufanikisha hayo yote, ODM ilihitaji mabilioni ya pesa.
Imefichuka chama hicho hakikujali mahali pesa hizo zingetoka kwani orodha ya wafadhili wao inajumuisha mataifa maskini ya Afrika yanayotambulika kwa ukatili dhidi ya raia ambapo rasilimali huliwa na matajiri wachache wenye ushawishi mamlakani.
Wafadhili wengine walijumuisha mhubiri mashuhuri ambaye anakumbwa na mashtaka ya ulanguzi wa binadamu. Vile vile, kuna wahariri wa vyombo vya habari ambao imefichuka walitumikia chama hicho ili kuwezesha ajenda za ODM kujikita akilini mwa raia.