Habari

Yafichuka vita Njoro si vya kisiasa pekee

August 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH OPENDA

UKOSEFU wa vyeti vya ardhi, hofu ya kutimuliwa na wizi wa mifugo ni kati ya masuala ambayo yametajwa kama yanayosababisha mapigano ya kila mara kati ya jamii mbili hasimu maeneo ya Molo na Njoro katika Kaunti ya Nakuru.

Jamii za Ogiek na Kipsigis ambazo zinaishi Marioshoni na Nessuit zimekuwa zikishiriki mapigano kutokana na mzozo wa ardhiOgiek ambao wanaishi msituni pia wamekuwa na hofu ya kuondolewa humo na maafisa wa serikali.

Tangu ghasia zizuke kati ya jamii hizo wiki jana, watu watano wamefariki, wengine 80 wakajeruhiwa huku zaidi ya 3,000 wakilazimika kuhama makwao.

Kipsigis wamekuwa wakiwalaumu Ogiek kwa kuwafurusha kwenye ardhi ambayo iliwauzia hasa baada ya serikali kutangaza kwamba itatwaa vipande vya ardhi za msitu ambavyo vimekaliwa na wanadamu.Mzee Daniel Lagat, 76 kutoka jamii ya Kipsigis alisimulia kuwa alinunua ardhi yake mnamo 1994 kutoka kwa mmoja wa jamii ya Ogiek.

Amekuwa akiishi na kushiriki kilimo kwenye kipande hicho cha ardhi.“Walipotuuzia ardhi, baadhi yao walisonga hadi ndani ya msitu na walipotakiwa waondoke, walianzisha vita.

Hii ni kwa sababu wanataka tuondoke ili wachukue vipande vya ardhi walizotuuzia,” akasema Bw Langat.? Anadai viongozi wa kisiasa pia wamekuwa wakifadhili makundi ya vijana yawavamie na kuteketeza nyumba za watu wanaotoka jamii ya Kipsigis.

Naye Jackson Kumare, kutoka jamii ya Ogiek anadai ghasia hizo zimesababishwa na wizi wa mifugo unaotekelezwa na jamii ya Kipsigis.

Bw Kumare alisema kuwa kila mara vijana Wakipsigis huwaibia mifugo na wanapokamata mshukiwa mmoja na kumpa kipigo, jamii hiyo hudai kwamba Ogiek wanalenga kuwafurusha kutoka kwa mashamba yao.

Alipuuza madai kwamba wanataka kuchukua ardhi waliyowauzia Wakipsigis, akisema jamii zote zimeathirika na oparesheni ya kuwaondoa msituni inayoendeshwa na serikali.

Anasema jamii ya Ogiek huondoka msituni kwa amani kila mara serikali inapowahitaji wafanye hivyo ila hali ni tofauti kwa Wakipsigis ambao huzua vita wakiambiwa waondoke msituni.

Bw Kumare pia alisema wanasiasa hutumia suala la kuondoka msituni kutimiza malengo yao ya kisiasaKamishina wa Bonde la Ufa George Natembeya kwenye mkutano ulioandaliwa katika kituo cha kibiashara cha Neissut alizitaka jamii zote mbili ziishi kwa amani na pia zisishiriki kwenye vita vikali kutokana na mzozo wa ardhi.

Bw Natembeya aliahidi kwamba serikali itaanzisha mikutano ya amani katika maeneo ya Nessuit na Marioshoni.