Habari za Kitaifa

HAKUNA PENSHENI: Wizara ya Fedha yashutumiwa kwa kuchelewesha malipo ya uzeeni

Na JOHN MUTUA August 23rd, 2024 1 min read

WIZARA ya Fedha imeendelea kuchelewesha malipo ya pensheni kwa wafanyakazi wa umma waliostaafu huku ikifeli kutoa pesa za Julai mwaka huu.

Hii ni licha ya kuwa jumla ya Sh223.15 bilioni zimetengwa katika bajeti ya serikali ya mwaka wa kifedha 2024/2025 kugharamia malipo ya pensheni ya wastaafu hao.

Kuchelewa huko kunaongeza madhila yao kwani hawakupokea Sh23.78 bilioni walizotengewa katika bajeti ya mwaka uliopita wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2024.

Wizara ya Fedha imezongwa na mzigo wa ulipaji madeni huku kiwango cha mapato yake kikipungua, hali ambayo imeifanya kushindwa kutoa pesa za pensheni kwa wakati.

Jumla ya wastaafu 259,222 na watu wengine 83,615 wanaotegemea pensheni hiyo kukimu mahitaji yao ya kila siku, wataathiriwa na uchefuchefu huo wa kifedha.

Bunge limeshutumu Wizara ya Fedhha kwa hali hiyo na sasa linapendekeza mageuzi makuu katika mchakato wa utoaji pensheni.

“Hatua za kisera zinazolenga kuleta mageuzi katika usimamizi wa rasilimali ziwekwe ili kupunguza mzigo wa ulipaji pensheni,” Kamati ya Bunge kuhusu Madeni ya Umma ilisema mwezi jana.

Baada ya kulipa madeni ya umma, ulipaji pensheni ndilo jukumu la pili ambalo Wizara ya Fedha inapasa kulipa kipaumbele.

Lakini mzigo mkubwa wa madeni na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kukosa kufikia kiwango lengwa cha ushuru inaokusanywa,  zimechangia kucheleweshwa kwa malipo ya uzeeni. Aidha, haijabainika iwapo Wizara ya Fedha imetoa pensheni tangu kuanza kwa mwezi huu.

Umri wa kustaafu kwa watumishi wa umma ni miaka 60. Mzigo wa malipo ya uzeeni unatarajiwa kuongezeka katika kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya Rais William Ruto kuagiza kwamba ni sharti kwa wafanyakazi wa serikali kustaafu wanapotimu miaka 60.