Makala

Harusi yageuka mazishi bi harusi alipofariki ghafla

Na MWANGI MUIRURI August 19th, 2024 2 min read

BAADA ya kuishi kwa ndoa isiyo rasmi na mkewe kwa miaka 26, Bw Stanley Macharia aliamua kuirasmisha mnamo Agosti 17 huku Kanisa la Kianglikana eneo la Pumwani, Nairobi, likipangwa kuwa mahali pa sherehe hiyo.

Alipaswa kurasmisha ndoa hiyo na mkewe, Nancy Muthoni, na kisha kuwafanyia sherehe waliohudhuria katika uwanja wa Shule ya Msingi ya St Anne kwenye Barabara ya Jogoo.

Kamati ya harusi ilikuwa imeundwa, kadi za mwaliko zilikuwa zimetumwa, washonaji wa mavazi walikuwa wamekamilisha kazi yao na mchungaji wa kuongoza harusi alikuwa tayari.

Mwanadamu hupanga, lakini Mungu huamua. Sherehe hiyo ya furaha haikufanyika baada ya Bi Muthoni kufariki siku 11 kabla ya siku hiyo kuu. Macharia, naye aliamua siku hiyo isingepita tu, aliamua kuwa siku ya harusi ingekuwa ya sherehe ya mazishi.

Bibi arusi mfu alivaa gauni

Ni uamuzi kama huo uliozua hafla ya kusikitisha Jumamosi katika kijiji cha Gikoe eneobunge la Mathioya, Murang’a. Wapambe wa maharusi, katika mazishi, walivalia mavazi ya harusi, huku bi harusi akiwa amelala kwenye jeneza lake akiwa amevalia gauni lake.

Umati uliofurika katika kanisa la ACK Gikoe ulikimya na kusikiliza kwa makini wanenaji, wakisimulia jinsi harusi hiyo ingekuwa kubwa, ya kupendeza na ya kuburudisha.

Mchungaji Margaret Muchiri aliyepaswa kusimamia ukataji keki harusini alisema kuwa harusi hiyo iliishia kuwa ya Bi Muthoni na Mungu.

“Harusi ya kidunia na mumewe haitakuw. Tunamuombea Bw Muchiri amngojee kwa subira Mungu afichue mipango yake kwa kuwa sasa alimemchukua mkewe,” akasema.

Macharia, akisema upweke na utupu uliotokana na kifo hicho utahitaji neema ya Mungu kushinda, anasema alitaka kurasmisha ndoa yake ya njoo tuishi kupata usalama wa siku zijazo enzi hizi za wajane kunyimwa urithi.

“Mwanamume anapozeeka, lazima aanze kupanga nyumba yake, kuoa mke wako rasmi ni sehemu ya maisha kwa kutarajia kuondoka kwetu kutoka kwa ulimwengu wa maisha. Ni aina ya usalama wa kijamii na kiuchumi kwa wote na watoto,” alisema.

Badala ya kubadilisha viapo, mjane alitoa heshima za mwisho kwa mwanamke ambaye kwa pamoja walikuwa wamezaa wana wawili, na mjukuu kama bonasi.

Bw Macharia pamoja na wanawe wawili walisoma risala zao ambazo zilimtambulisha marehemu kama mwanamke aliyeipenda familia yake.

Alitajwa kuwa mchapakazi na mwenye bidii kiasi kwamba pengo aliloacha litawatesa kwa muda.

Kamati andalizi ilijaribu kadiri iwezavyo kuipa sherehe ya mazishi sura ya harusi, lakini machozi ya huzuni hayakuweza kuwa kama yale ya furaha.

Bi Nancy Mwangi ambaye angekuwa mpambe wa bi harusi katika harusi hiyo alitokwa na machozi mashavuni mwake lakini akajaribu sana kuongea kwa furaha.

“Tuliamua kuvaa mavazi yote ya harusi kama ilivyokuwa imepangwa kwa sababu leo ni siku ya harusi kwa rafiki yetu aliyefariki, natangaza furaha katika maumivu haya na nina hakika amefurahi kuwa siku hiyo imefika,” alisema.

Wazungumzaji wakati wa hafla ya mazishi walizungumza kuhusu mipango ya Mungu inavyoshinda ya mwanadamu.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya harusi Bw John Ng’ang’a alisimulia jinsi kamati hiyo iliyokuwa ikiandaa harusi iliamua haitavunjwa baada ya kifo cha Bi Muthoni na ikaaanza kuandaa mazishi.