Habari

Hukumu: Esther Arunga apata afueni

July 18th, 2019 1 min read

Na AGEWA WAINAINA

ALIYEKUWA mtangazaji wa televisheni, Bi Esther Arunga amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi 10 jela baada ya kukiri Jumatatu kwamba alidanganya kuhusu hali na mazingira ambamo mumewe, Quincy Timberlake alimgonga marehemu mwanawe.

Hata hivyo, Jaji amemuachilia mara moja kwa masharti kwamba ataonyesha tabia na mwenendo mzuri.

Katika uamuzi wake wa Alhamisi, Jaji Martin Burns amenukuliwa na Australian Associated Press akisema amezingatia sana mazingira ya huzuni yaliomzingira alipozungumza na maafisa waliokuwa wanapeleleza kifo cha mwanawe.

“Inachukuliwa kwamba ulikuwa kwa mshtuko mkubwa baada ya kifo cha kijana wako wakati ulihojiwa pamoja na kwamba ulikuwa unaomboleza,” amesema Jaji.

Jaji amehitimisha kwamba imani za kiutamaduni za Arunga zilichangia na kwamba tangu mwaka 2014 hadi 2019 akihukumiwa tayari alikuwa amepitia “machungu mengi”.

“Ulikuwa mke, mama aliyekuwa akimtunza mtoto mwenye umri wa miezi sita tu, na kwa kipindi hicho ukijaribu kustawisha familia yako katika nchi geni hadi kufikia kumpoteza mtoto wa kiume, mume, na mabinti,” amesema Jaji.

Awali Arunga akikuwa ametoa ushahidi kwamba mumewe alikuwa amemgonga mwana wao Sinclair Timberlake aliyekuwa na umri wa miaka mitatu “kumwokoa kutoka kwa shambulizi la mapepo.”

Bi Arunga alishtakiwa kwa kumsaidia katika mauaji ya mwana wao Sinclair Timberlake aliyekuwa na umri wa miaka mitatu.

Alisema alifanya hivyo kumwokoa mumewe.

Sinclair alifariki baada ya maumivu yaliyosababishwa na kifaa butu tumboni mwaka 2014 katika nyumba yao mjini Kallangur, Australia.