Habari za Kitaifa

IG Koome azidiwa na presha ya Gen Z, akanyaga kubwa kubwa

Na BENSON MATHEKA July 12th, 2024 1 min read

INSPEKTA Jenerali wa polisi Japhet Koome amezidiwa na presha kutoka wa umma na kujiuzulu, Rais William Ruto ametangaza.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Koome aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais.

“Mheshimiwa William Samoei Ruto, Ph.D, CGH, Rais na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, mnamo  Julai 12 2024, amekubali kujiuzulu kwa   Mhandisi Japheth N Koome, MGH, kama Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi,”  ilisema taarifa hiyo.

Rais amemteua Douglas Kanja kuwa kaimu Inspekta-Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa. Kanja alikuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi.

Bw Eliud Langat atakuwa Kaimu Naibu Inspekta Jenerali, Huduma ya Polisi ya Kenya huku Bw James Kamau akiwa Kaimu Naibu Inspekta Jenerali, Huduma ya Polisi wa utawala.

Kumekuwa na shinikizo za kutaka Koome ajiuzulu kutoka kwa vijana ambao wamekuwa wakiandamana hasa baada ya watu kadhaa kuuawa kwa risasi na vitoa machozi, kutekwa nyara na polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao hawakuwa wamevunja sheria.