Habari za Kitaifa

Jiandaeni kwa juma lenye mvua na baridi kali – Idara ya Utabiri

Na BENSON MATHEKA July 31st, 2024 1 min read

WAKENYA wameshauriwa kujiandaa kwa mvua kubwa na baridi kali katika baadhi ya maeneo katika kipindi cha siku saba zijazo.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya imetabiri kuwa mvua kubwa itanyesha kuanzia Julai 30 hadi Agosti 5 katika baadhi ya maeneo ikiwemo Kaunti ya Nairobi.

Katika utabiri wake, idara hiyo ilisema kuwa baadhi ya maeneo nchini yatapokea mvua kubwa na ya wastani.

Miongoni mwa maeneo yanayotabiriwa kupata mvua ni pamoja na Nyanda za Juu za Kati, Magharibi mwa Kenya, Bonde la Ufa, Kaskazini-magharibi mwa Kenya, na Pwani.

Kaunti za maeneo haya ni pamoja na Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi.

Kaunti nyingine ni pamoja na Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru.

Kaunti za Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi zinatarajiwa kupata mvua kubwa kwa siku tano zijazo.

“Vipindi vya jua vinatarajiwa wakati wa mchana hali usiku huenda kukawa na mawingu kiasi ingawa mara kwa mara manyunyu na ngurumo za radi zinaweza kutokea katika maeneo machache,” idara hiyo ilitangaza.

Wakati huo huo, sehemu nyingine za nchi zinatarajiwa kubaki kavu kwa jumla huku hali ya jua ikitarajiwa katika maeneo mbalimbali.

Wakenya wanaoishi katika kaunti zilizotajwa hapo juu pia walionywa kuhusu majira ya baridi kali ya usiku ya chini ya nyusi 10.

Kaunti zinazotarajiwa kupata viwango vya juu vya joto mchana ni pamoja na; Mombasa, Tana-River, Kilifi, Lamu, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa Isiolo na Kwale.

“Hali ya baridi na mawingu inatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu za eneo la Kati, Magharibi mwa Kenya, nyanda za chini Kusini-mashariki na Bonde la Ufa,” idara ilisema.