Makala

Jina ‘Pokot Magharibi’ ni bandia, sio letu; libadilishwe – Wazee

Na OSCAR KAKAI July 17th, 2024 3 min read

WAZEE kutoka jamii ya Pokot sasa wanataka jina ‘Pokot Magharibi’  kubadilishwa na kuitwa jina asilia. 

Awali, wilaya ya Pokot Magharibi ilikuwa inaitwa, West West Suk ama Wilaya ya Kacheliba na ilikuwa katika mkoa wa Bonde la ufa, Kenya.

Haya yanajiri baada ya tume ya uwiano na utangamano (NCIC) kupendekeza kubadilisha majina ya kaunti kumi ikiwemo Pokot Magharibi.

Kaunti zingine ni Meru, Tharaka Nithi, Nandi, Kisii, Turkana, Embu, Samburu, Taita Taveta, na Elgeyo Marakwet ambazo zimetambuliwa kuwa majina ya ukabila

Tume ya NCIC itawasilisha mswada kwenye bunge kubadilisha majina hayo.

Kaunti ya Pokot Magharibi imejulikana kwa mambo mazuri na hata mabaya.

Mji wa Kapenguria ambao ndio makao makuu ya Kaunti ya Pokot Magharibi. Picha|Oscar Kakai

Makao yake makuu ni mjini. Kaunti hiyo ina ukubwa wa skwea kilomita 9,169.4 na upana wa kilomita 132 kutoka Kaskazini hadi Kusini.

Kaunti ya Pokot Magharibi inapakana na Kaunti ya Turkana upande wa Kaskazini, Baringo upande wa Mashairiki na Kusini Mashariki ni Kaunti ya Elgeyo-Marakwet, Kusini ni Kaunti ya Trans-Nzoia na Magharibi ni Uganda. Kulingana na sensa ya mwaka wa  2019, kaunti hiyo ina idadi ya watu 621,241.

Kaunti hiyo imekuwa ikigonga vichwa vya habari kuhusiana na ujangili na wizi wa mifugo.

Jina la Pokot Magharibi lilianza mwaka wa 1952.

Aliyekuwa Meya wa Kapenguria Christopher Lonyala anasema kuwa Kaunti ya Pokot Magharibi ilikuwa inaitwa Wilaya ya West Suk.

Anasema kuwa jina hilo lilibadilishwa mwaka wa 1952 na aliyekuwa naibu wa waziri marehemu James Koreliach ambaye alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapenguria.

Anasema kuwa wilaya hiyo ilikuwa Uganda kabla ya kuletwa Kenya mwaka wa 1902 na kuja Kenya mwaka wa 1970.

Bw Lonyala anasema kuwa wametuma malalamishi yao kwa bunge la Seneti kuhusu suala hilo.

Mbunge wa kwanza wa Wilaya ya Pokot Magharibi Jacob Lorema wakati wa mahojiano. Picha|Oscar Kakai

“Wilaya ya Sook ilikuwa katika mkoa wa  Naivasha. Pokot Magharibi sio jina letu. Ni jina bandia. Angali kwa ramani zetu na vile wazungu waliandakika. Eneo la Suk linaaanzisha Moroto hadi Ziwa Baringo.  Lazima turejeshe jina letu la mababu ambalo tulipewa na Mungu. Hata samba hupewa majina lakini hawajui wanaitwa hivyo. Suk, Karamoja, Mathaniko, Sebei na Turkana zilikuwa kwenye mkoa moja,”alisema.

Alisema kuwa Pokot Magharibi ambayo ni kaunti 024 inafaa kupewa jina lake la kaunti ya West Suk.

“Tunaunga mkono kubalishwa kwa jina. Jina la Pokot Magharibi limechafuliwa na serikali kuwa sisi ni wezi wa mifugo. Wilaya ya West Suk ilikuwa ya amani mwaka wa 1952 ndio sababu Jomo Kenyatta na wenzake waliletwa kufungwa hapa. Wazungu walifunga wilaya katika eneo la Keringet. Jina Pokot Magharibi ni jina bandia na halituhusu. Koreliach alikuwa akiongea kizungu na wazungu baada ya kutoka kusoma Kakamega akishirikiana na marehemu Lubae na Maket,” anasema.

Anasema kuwa makao makuu ya wilaya hiyo ilikuwa Kacheliba mwaka wa 1952 kisha ikakuja Kapenguria.

Stephen Cheselokwot Loriareng, mzee kutoka eneo la Batei anasema ni vyema jina hilo kubadilishwa.

“Inafaa kubadilishwa kutoka kaunt ya Pokot Magharibi iwe kaunti ya Pokot ili iwe na jina na watu wake ama iwe kaunti ya Kapenguria,” anasema.

Mbunge wa kwanza wa Wilaya ya Pokot Magharibi Jacob Lorema naye alipinga suala hilo akisema kuwa jina hilo linafaa kusalia hivyo kabla ya kuhamasisha wakazi kupeana maoni yao.

Anasema kuwa kaunti ya Pokot Magharibi ni ya amani.

“Jina hilo liliharibiwa na wanabiashara ambao walikuwa wanataka kutawala kibiashara. Walikuwa wanaogopesha wanabiashara wengine wasije kufanya kazi wakati wanafika Kitale sababu walitaka kufanya biashara pekee yao. Eneo hili ni salama. Mji wa Kapenguria una kila kabila. Tunakaribisha kila mtu na wale wanasema kuwa sisi ni wabaya ni waongo,” anasema.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magahribi Simon Kachapin ambaye aliongea na Taifa Leo kwa njia ya simu anazsema kuwa suala na kubadilisha jina la kaunti ni nzuri lakini lazima wakazi watoe maoni na wahamasishwe.

“Sio jambo la kuamka tu na kubadilisha. Lazima uhusishe washikadau.” alisema.

Anasema kuwa Kaunti ya Pokot Magharibi imeorodheshwa kati ya kaunti ambazo hazina ujangili mwingi.

“Asilimia 95 ya Pokot Magharibi ni salama isipokuwa maeneo machache ya  Turkwel na Chesegon,” alisema Bw Kachapin.

Mwakilishi mtuele wa wadi Marishana Cheruto aliunga mkono suala hilo.