Habari za Kaunti

Jinsi ukosefu wa sodo Pokot Magharibi unachangia wasichana kuacha shule

April 1st, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI 

KAUNTI ya Pokot Magharibi ingali inakumbwa na kero ya uhaba wa tauli za hedhi hususan kwa wasichana wa shule, suala ambalo linawapitishia changamoto kibao.

Wengi wanaishia kuacha masomo, na kujitosa kwenye ndoa za mapema.

Bidhaa hiyo muhimu ya kimsingi ikiendelea kuwa adimu, waathiriwa wanakosa kuenda shuleni kwa kuona aibu kipindi cha hedhi.

Umaskini na ukosefu wa hamasisho kuhusu manufaa ya taulo za hedhi, umebainika kuwa chanzo kikuu cha mahangaiko kwa wasichana wadogo (walioanza kupata hedhi) na kina mama.

Pia sodo, taulo ni bidhaa malum inayotumiwa na jinsia ya kike wakati wa mzunguko wa utokaji damu – hedhi.

Aidha, uhaba wa bidhaa hiyo Pokot Magharibi unashinikiza wasichana na wanawake kutumia ‘vifaa’ vichafu kama vile vipande vya godoro, gazeti, viraka, majani yaliyokauka au soksi.

Wengi wanakosa kupata taulo za hedhi kwa ajili ya ufukara, wasichana wakiishia kuhadaiwa na wanaume wahuni hivyo basi kuacha masomo.

Isitoshe, kwa walio shuleni wanakosa morali kukata kiu cha masomo.

Hii ni kutokana na aibu ya kutokwa na damu, uchungu ama kukosa amani wakati wa hedhi.

Serikali ya kitaifa ilikuwa imeahidi wabunge wawakilishi wa kike kima cha Sh940 milioni, na kufikia sasa haijaafikia ahadi hiyo – kwa kiwango kikubwa ikilaumiwa kufuatia mahangaiko ya wasichana kukosa sodo.

Kenya ina kaunti 47, kila moja ikiwa na mwakilishi wa kike kutetea jinsia ya kike bungeni.

Wabunge kutoka Pokot Magharibi sasa wanamtaka Waziri wa Jinsia, Aisha Jumwa kushinikiza utoaji wa fedha zilizoahidiwa na serikali.

Mwakilishi wa kike Pokot Magharibi Bi Rael Kasiwai na mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto ambao wamelalamikia kuhusu kucheleshwa kwa fedha hizo, wanasema kuwa wasichana katika maeneo ya mashinani wanaumia sana.

Wanateta maeneo ya jamii za wafugaji yameishi kutengwa na kusahaulika kwa muda mrefu, hasa katika ugavi wa raslimali.

Bi Kasiwai anaitaka serikali kuu na mashirika ya kijamii kusaidia wasichana maeneo ya wafugaji ili waweze kusoma vyema.

Anasema kuwa hali inaendelea kuwa mbaya zaidi mashinani, jambo analohoji kama watetezi wa wananchi bungeni hawana subira tena.

“Hedhi sio chaguo kwa wasichana wa mashinani na Kenya nzima. Ni hatua ya kila mwanamke maishani,” anasema.

Bi Kasiwai anaitaka serikali kuweka mikakati maalum kuangazia changamoto zinazofika wanawake katika maeneo ya jamii za wafugaji.

“Wasichana wengi wako nyumbani kwa sababu ya ukosefu sodo. Wameshindwa kuenda shule,” anasema Bi Kasiwai.

Aidha, anatoa wito kwa viongozi kuingilia kati suala hilo akisema kuwa limeathiri elimu ya mtoto wa kike Pokot Magharibi.

Mbunge huyo anataka serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi kutenga fedha kununua sodo na kuzisambaza shuleni, kupitia makadirio yake ya bajeti kila mwaka.

“Sodo moja huku ni Sh50 na wasichana huzitumia kila wakati wa hedhi,” aliambia Taifa Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Anapendekeza kiwango fulani cha mgao wa ustawishaji maeneobunge (NG-CDF) kutumika kununulia wasichana taulo za hedhi.

Naye mbunge wa Kapenguria, Bw Samuel Moroto anasema kuwa wazazi wengi eneobunge lake hawafahamu umuhimu wa sodo, huku wengine wakikosa hela kununua bidhaa hiyo muhimu ya kimsingi kwa jinsia ya kike.

“Wazazi wengi hawajasoma na hawaoni umuhimu wa taulo hizo za usafi. Serikali kuu na kaunti zinapaswa kuingilia kati ili wasichana wapate sodo,” anasema.

Anasema kuwa shule nyingi Pokot Magharibi ni za mseto, na kwamba wasichana huwa na hofu kuenda shuleni wanapopokea hedhi.

“Inasikitisha kuona baadhi ya maeneo unaweza kutembea zaidi ya kilimota 50 ili kupata duka lenye sodo,” Bw Moroto anasema.

Mbunge huyu anasema baadhi ya wazazi wanatumia mwanya huo kuoza binti zao mapema ili kuondokea umaskini.

“Si ajabu upate mzazi ‘akiuza’ bintiye kwa ng’omnbe 20. Ni aibu kutoa motto shule akaoleke”.

Mwalimu mkuu Shule ya Upili ya Wasichana ya Puropoi Jamas Murray, anasisitiza haja ya wasichana kusaidiwa kudumisha usafi wakati wa hedhi.

“Uchafu hufanya wengi kujidharau na wanakosa kuja shule,” anasikitika.