Makala

Jinsi ushoga umegeuzwa ufisadi wa mamilioni Kenya

January 9th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

Habari zinazochipuka katika mjadala mkali unaoendelea kuhusu kukubalika kwa ushoga na usagaji nchini ni kwamba hali hizo za mahaba zinazosutwa na wengi kuwa dhambi zimegeuzwa kuwa ufisadi mkuu wa mamilioni.

Kumeanza kueleweka kwamba kuna wanaume na wanawake hasa wa umri wa ujana ambao wako katika hali hizo kujipa riziki tu na baada ya kulipwa, wanakimbia kwa husiano zao za kawaida kujipa raha.

Vijana hao huwa wako katika husiano za kawaida lakini wanatoa huduma za ushoga na usagaji ili walipwe ndio waweze kufadhili maisha yao ya kawaida.

Martin Ndung’u ambaye hushirikisha harakati za mashoga mjini Thika aliambia Taifa Leo kwamba “hii ni hali ambayo imegeuzwa kuwa ufisadi mkuu na uaherati wa hali ya juu ambapo wengi hawako ndani ya ushirika wetu kwa dhati mbali ni matapeli”.

Alisema kwamba hata kumeibuka mashirika ya kijamii (CBO) na yasiyo ya kiserikali (NGO) ambao wanasajili wanachama bandia ili wapate ufadhili kutoka Ulaya.

“Tunaona mikutano ikiandaliwa eti ni ya mashoga na wasagaji na unapata mabwana na mabibi zao wakihudhuria ili wapate marupurupu na washirikishi wanapata mamilioni,” akasema.

Aliongeza kwamba ukijisajili kama shoga au msagaji katika makundi hayo, unawekwa katika mpango wa kiinua mgongo cha kila mwisho wa mwezi hivyo basi kuvutia hata wasio ndani ya hali hizo kama mwito wa kihisia.

Alisema huenda ihitajike kuwe na kuhesabiwa kwa mashoga na wasagaji iwapo serikali itakubali kusajili muungano wao kama ilivyoamrishwa na mahakama hivi majuzi.

“Mimi nilichanuliwa na rafiki yangu kwamba ningejipa pesa tamu iwapo ningekubali kuwa mke wa wakubwa fulani. Nilielezewa kwamba kutekelezewa ushoga kwa masaa matatu ningepata Sh100,000. Nilishawishika kukubali,” asema kijana mmoja kutoka Murang’a.

Anasema sasa huu ni mwaka wake wa pili katika biashara hiyo na ameweza kujinunulia gari na kuanza biashara ya uuzaji wa viatu licha ya kuwa ako katika mwaka wa pili katika chuo kikuu kimoja nchini.

Anasema kwamba wateja wake huwa wafanyabiashara, wanasiasa na hata wachungaji.

Ingawa mwenyekiti wa baraza la Agikuyu Bw Wachira Kiago anataja ushoga na usagaji kama mwiko katika jamii hiyo, kijana huyo wa Murang’a anasema kwamba “mwiko wa kimila na wingi wa pesa wewe utachagua gani?”

Kijana mwingine kutoka Thika aliambia Taifa Leo kwamba, “mimi niko na mpenzi wangu wa kike na ambaye ako na mimba yangu lakini ndio nimtunze huwa naitiwa kazi ya ushoga na mabwanyenye fulani Nairobi”.

Msichana tuliyekumbana naye katika mkahawa mmoja Kaunti ya Embu alikiri kuwa na watoto wawili ndani ya uhusiano unaoendelea hata sasa na mwanamume “lakini kwa usagaji niko kikazi”.

Alisema kwamba kuna wanawake walio na pesa na huwa wanahitaji wanawake wa kuwapapasa na kuwaamshia hisia zao za kimahaba hadi kilele.

“Ilibidi kwanza nisake wasagaji wa ukweli wanifunze vile hali huwa na kwa sasa nimekuwa mweledi wa kuwafikisha wasagaji kilele. Nikishalipwa, nakimbia kwa mume wangu,” akasema.

Alisema kwamba kinyume na hatari ya kuraruliwa ambayo huwaandama wanaume, kwa wanawake hakuna hesabu nyingi za madhara.

Katika hali hiyo, wengi wa mashoga na wasagaji wanadai kueleweka ipasavyo na mjadala huo utenganishe mashoga na wasagaji halisi na wenzao ambao wako kazi nyoyo zao zikiwa bado kwa mapenzi ya kawaida.

[email protected]