Habari Mseto

Kanisa lenye historia ya vurugu kupiga msasa maaskofu

January 15th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

KIONGOZI wa African Independent Pentecostal Churches of Africa (AIPCA) Askofu Mkuu Samson Muthuri ametangaza msasa wa maaskofu walio chini yake ili kuwatema wasiofaa.

Askofu Muthuri alichaguliwa mwishoni mwa 2023 kuongoza kanisa hilo ambalo kwa miaka 20 sasa limekuwa ndani ya mgogoro wa uongozi.

Migogoro hiyo ilikuwa ikijidhihirisha katika visa vya waumini kuvamiana kwa mangumi na mateke na pia kushambuliana kwa maneno makali kwenye madhabahu.

Mzozo huo uliingiliwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na akaweka viongozi wa mirengo mitatu kubadilishana uongozi kwa awamu ya mwaka mmoja kwa kila mmoja wao.

Baada ya kuondoka mamlakani 2022, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alirithi jukumu hilo la upatanishi hadi kukaandaliwa uchaguzi na Askofu Muthuri ambaye alimwangusha mpinzani wake wa jadi Askofu Frederick Wang’ombe.

Askofu Muthuri sasa, majaliwa, atakuwa katika uongozi wa kanisa hilo hadi mwisho wa 2026 ambapo uchaguzi mwingine utaandaliwa.

Sasa, katika hali inayoonekana ya kujidhibiti mamlakani na kuwang’oa ‘wasiofaa’, Askofu Muthuri ametangaza kuwa msasa huo wa wadogo wake utaanza Januari 19, 2024.

“Zoezi hili ni kwa mujibu wa Katiba yetu ya AIPCA ambayo tumepitisha hivi majuzi. Msasa huo unahitaji kila Askofu afike mbele ya jopo akiwa na stakabadhi zake za elimu, kitambulisho cha kitaifa, na orodha ya makanisa yaliyo chini yake,” tangazo lake kwa maaskofu hao linasema.

Hatua hii imezua wasiwasi miongoni mwa kanisa hilo ambalo lina historia ya kushirikisha vita vya uhuru wa taifa hili.

“Tunafuatilia kwa makini sana harakati hizi za Askofu huyu mpya. Bado tuna shaka kuu kuhusu masuala ya kuchaguliwa kwake kwa kuwa kunao tunaoamini kwamba muingilio wa siasa za Mlima Kenya ulishawishi matokeo. Isiwe sasa msasa huo ni wa kisiasa,” akasema mmoja wa maaskofu hao.

Aliongeza kwamba “mzozo wa uongozi huwa unazingatia maeneo ya Mlima Kenya ambapo kuna mrengo wa Mashariki ukijumuisha Ameru ukishindania udhibiti na eneo la Kati mwa nchi”.

[email protected]