Habari za Kaunti

Kanjo feki watawala Nairobi tangu Sakaja kuwa Gavana 

Na KEVIN CHERUIYOT September 3rd, 2024 2 min read

WAFANYABIASHARA katika Kaunti ya Nairobi wamelalamikia kuhangaishwa na watu wanaodai ni askari wa jiji ilhali hawajaajiriwa na utawala wa kaunti.

Tangu Bw Sakaja aingie afisini baada ya kushinda uchaguzi wa 2022, wafanyabiashara wanadai wamekuwa wakihangaishwa na watu ambao wanajidai ni kanjo.

Kwao imekuwa vigumu kubaini nani ni kanjo halali huku wakiendelea kuandamwa kila wanapofanya biashara, baadhi hata wakikamatwa na kulazimishwa kutoa pesa kabla ya kuachiliwa.

Elizabeth Mwangi amekuwa mchuuzi jijini Nairobi kwa zaidi ya miaka 20.

Katika kipindi hicho, amepambana na changamoto nyingi, ikiwemo kuibiwa mchana peupe, kuhangaishwa na polisi, kufurushwa na biashara zake kukosa kutambulika.

Bi Mwangi anasema kuwa watu ambao wanajifanya kanjo wamekuwa wakiwasumbua, hawavalii sare rasmi wala hawana vitambulisho vinavyoonyesha kuwa wao ni kanjo.

“Ninawajua wale feki na wale wa kawaida na hawawezi kugusa bidhaa zangu. Nimewaona baadhi yao wakiwanyanyasa na kuwahangaisha wafanyabiashara wenzangu,” akasema Bi Mwangi.

Wiki jana, Julius Nzioki alikuwa akiuza bidhaa zake kwenye barabara ya Latema wanaume wawili ambao walidai walikuwa kanjo walipofika.

Walimtia pingu, kabla ya kuanza kuzunguka naye kwenye barabara kadhaa jijini, huku wakimwitisha hela.

“Waliniacha baada ya muda wa saa moja,” akasema Bw Nzioki.

Inadaiwa askari hao feki huwa wanalenga zaidi wachuuzi 6,000 ambao wamesajiliwa na City Hall na maelfu ya wengine ambao wanafanya biashara bila leseni.

Maeno ambayo kanjo hao feki wamezoea kuwanyanyasia wafanyabiashara ni OTC, Riverside, kituo cha mabasi cha Central, mzunguko wa Khoja, Fire Station, River Road, Latema, Tom Mbota, pamoja na kituo cha mabasi cha Embasava.

Wengi wa wachuuzi walisema kuwa kanjo hao feki walianza kuwahangaisha baada ya utawala wa Mkurugenzi wa Huduma za Jiji Mohamed Badi kukamilika.

Walitua barabarani kwa kishindo baada ya Bw Sakaja kushinda ugavana mnamo Agosti 2022.

Kufuatia kuondoka kwa NMS, kandarasi ya kazi za maafisa 700 wa jiji zilifutiliwa mbali baada ya Bunge la Kaunti ya Nairobi kupinga wao kuajiriwa na kaunti.

Baadhi ya maafisa hao ambao kandarasi zao zilifutwa ndio duru zinaarifu kuwa wanaendelea kusumbua wafanyabiashara kwa kuhudumu kama kanjo nje ya sheria. Baadhi hata walikataa kurudisha sare na pingu ambazo walikuwa nazo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wachuuzi Starehe, John Wamawaya alisema kuwa kanjo hao feki wanajulikana na wanashirikiana na wale wanaohudumu City Hall kisha kugawana hongo wanazokusanya kutoka kwa wafanyabiashara.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo