Habari za Kitaifa

Kemikali kuua wadudu zinasababisha aina sita ya Kansa

Na MERCY CHELANGAT August 7th, 2024 2 min read

IMEBAINIKA kuwa kemikali za kuua wadudu ambazo zimeidhinishwa kwa matumizi hapa nchini, zina sumu zinazosababisha aina sita ya kansa.

Licha ya matumizi yao kuidhinishwa na Bodi ya Kudhibiti Kemikali za Kuwaua Wadudu (PCPB), imebainika kuwa sumu hizo zinasababisha kansa ya mapafu, ya koloni, kongosho, kibofu cha mkojo, leukemia na ile inayofahamika kama non-Hodgkins lymphoma.

Sumu hizo zipo katika kemikali zinazotumika kuua wadudu wanaovamia mashamba ya mahindi, vitunguu, miwa, chai, ngano, maharagwe na nyanya.

Kwenye utafiti ambao ulichapishwa katika jarida la Frontiers Cancer Control Society, wataalamu wa afya walibaini kuwa sumu hii ni hatari na huumiza sehemu ya mwili.

Aidha sumu hiyo huangamiza chembechembe za DNA na kuathiri jeni mwilini. Pia, huchangia baadhi ya seli kubadilika na kuwa hatari kisha kusababisha kansa.

Hatari ya mwanzo inaweza kutokea wakati ambapo mkulima au mtu yeyote atakula au kunywa maji ambayo yana kemikali hatari ya kuua wadudu.

Hatari hiyo hutegemea sumu ya kemikali hiyo, hali ya anga, jinsi kemikali hiyo ilivyotumika na muda ambao makali ya kemikali hiyo hukithiri baada ya matumizi yake.

Kwenye tafiti za awali, kuna baadhi ya kemikali za kuua wadudu ambazo zimehusishwa na kansa ila kwenye utafiti huu ilibanika kuna mchanganyiko wa kemikali hizo hasa zinazonyunyiziwa au kuwekwa kwa mimea.

Ingawa hivyo, hatari hiyo haijashuhudiwa kwenye mahali ambapo kemikali hiyo ya kuua wadudu imetumika pekee kwa kuwa inaweza kusambaza katika maeneo mengine kupitia upepo au kusombwa kwa maji.

Wanasayansi waliozamia utafiti huo walihusisha lymphoma, aina ya kansa ambayo hulemaza kinga mwilini, kansa ya koloni na ile ya kongosho kama zinazosababishwa na kemikali hatari ya kuua wadudu yenye sumu inayofahamika kama glyphosate.

Kwa mujibu wa PCPB, kemikali ya glyphosate hutumika sana kudhibiti magugu kabla ya msimu wa upanzi. Pia hutumika sana kuzuia nyasi kumea katika mashamba ya majanichai.

Aina nyingine ya sumu ni Atrazine ambayo ni hatari na humweka mtu kwenye hatari ya kupata aina hizo sita za kansa. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeorodhesha Atrazine kama kemikali hatari zaidi wakati wa matumizi yake kukausha magugu kwenye mashamba ya mahindi.

Ibrahim Macharia, Mhadhiri wa Kitivo cha Kilimo na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta anasema kuwa wakulima hupatikana na matatizo mbalimbali ya kiafya kando na kansa baada ya kutumia kemikali hatari.

Kati ya matatizo ni pamoja na upigaji chafya, kichwa kuwaumiza, kutoona vizuri, ngozi kuwasha na pia kutatizika kuona.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo