Makala

KIKOLEZO: Sema busu kuyeyusha dili!

May 31st, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

TASNIA ya uigizaji huja na changamoto zake ambazo huwachanganya waigizaji kwani kando na kuvalia uhusika, nao pia wana hulka zao binafsi.

Mojawepo ya changamoto hizo ambazo zimetesa waigizaji kibao kote duniani, ni suala la kupigana busu na wenzao laivu kwenye kamera wakati wa uandaaji wa filamu au kipindi cha televisheni.

Ijapokuwa trendi hii ya kupigana busu kwenye filamu ilianza zama zile 1896 ikitokea mara ya kwanza kwenye filamu fupi ya dakika 25 iliyoandaliwa na Thomas Edison na kuifanya hadhira kuchukulia kawaida, kwa baadhi ya mastaa waigizaji, mpaka sasa imesalia kuwa mtihani mgumu.

Wapo wengi wao waliogoma kubadilishana mate na waigizaji wenzao wakati wa shuti. Kunao waliogoma kutokana na imani zao, wengine kutokana na heshima walizonazo kwa mahusiano yao kati ya sababu zinginezo. Ni misimamo mikali ambayo imewapelekea baadhi yao kupoteza dili kubwa kubwa. Hata hapa nyumbani pia wapo.

Lindsay Lohan

Kwenye uandaaji wa filamu ya komedi Scary Movie 5, 2013 mwigizaji Lindsay alitakiwa kumpiga busu mara tatu mwigizaji staa Charlie Sheen katika shuti tofauti tofauti.

Hata hivyo aligoma kutokana na historia ndefu ya Sheen kupenda mademu hivyo alihofia afya yake. Ililazimu maprodusa kutumia mbadala wa kinyago kilichofananishwa na Sheen kwenye sehemu hizo.

Sheen alipata umaarufu mkubwa kupitia series ya Two and Half Men. Miaka minne baadaye Sheen alitangaza kuwa ni mwathirika wa gonjwa la Ukimwi, alilopata kutokana na mahusiano yake na zaidi ya wanawake 1,000 katika maisha yake.

Nyce Wanjeri

Umaarufu wake aliupata kupitia kipindi cha Auntie Boss na kwa sasa Nyce ni miongoni mwa waigizaji wa kike wakubwa hapa nchini.

Japo anaweza kuvalia uhusika wowote ule, kitu kimoja ambacho kamwe hawezi kukubali ni pale uhusika huo utamtaka apigane denda na staa mwenzake. Yupo radhi kupoteza dili hiyo. Kwa Nyce ni vigumu sana kwake kubadilisha mate na mtu asiye na uhusiano naye.

“Hilo la busu kwenye kamera hapana, samahani siwezi. Ndio, mimi ni mwigizaji lakini kuna vitu ambavyo siwezi kufanya, vipo nje ya uwezo wangu. Ikitokea, itanifanya kujuta maisha yangu. Kila uhusika unaopewa huwa ni fursa ya kuwa mtu tofauti, lakini pia tusisahau kuwa katika hilo pia kuna hulka yako asili,” Nyce kaweka wazi.

Denzel Washington

Hivi ni nani anayeweza kugomea fursa ya kumpiga busu Julia Roberts mmoja wa waigizaji stadi wa kike duniani, kama sio Denzel pekee.

Denzel ametokea kwenye filamu kibao ambazo ameonekana kupigana denda, ila kwenye filamu ya The Pelican Brief 1993 aligoma kumpiga busu Julia wakati wakiigiza.

Mwigizaji Denzel Washington. Picha/ Hisani

Alisema msimamo wake ulitokana na sababu kwamba hakutaka kuwakwaza wanawake wenye asili nyeusi kwa kumpiga busu Julia ambaye ni mzungu.

Denzel alisisitiza kuwa idadi kubwa ya mashabiki wake ni wanawake weusi hivyo kumpiga busu Julia kungemchomea picha na kuwakwaza jambo alilotaka kuepukana nalo. Julia alinukuliwa akisema alitamani sana kumbusu Denzel ila alimgomea.

Janet Jackson

Kwenye uandaaji wa filamu ya kimapenzi Poetic Justice, mhusika mkuu Janet aligoma kumpiga busu marehemu rapa Tupac Shakur ambaye aliigiza kama mmoja wa wapenzi wake.

Janet aliomba kwanza Tupac apitie vipimo vya Ukimwi kabla ya kuendelea na uandaaji wa filamu hiyo. Uamuzi huo alisema aliuchukua kutokana na Tupac kuwapenda mabinti kupita maelezo.

Janet Jackson. Picha/ Maktaba

Japo Tupac alifanya hivyo na kisha kuelezea kuvunjwa moyo na hatua hiyo.

Janet alijitetea kwa kusema kwamba miaka hiyo, ugonjwa huo ulikuwa bado mpya na kulikuwepo na unyanyapaa kwa walioathiriwa kiasi cha kumwogopesha yeyote.

 

Neal McDonough

Ni mwigizaji mkubwa anayetambulika akiwa ametokea kwenye filamu na Series kibao zilizoweza kufanya vizuri kama vile Arrow, Desperate Housewives, Suits, Captain America: First Avengers kati ya zingine.

Kwenye filamu kibao alizotokea, amevalia uhusika wa muuaji.

Sharti moja alilonalo kwa produsa mmoja anayempa kazi ni kutompa uhusika utakaomtaka apigane busu au kushiriki kwenye sehemu za kimapenzi.

Neal McDonough. Picha/ Hisani

McDonough ni Mkatoliki mwenye imani kali. Hawezi kumpiga busu mtu yeyote zaidi ya mke wake wa ndoa.

“Siwezi kumpiga busu mwanamke yeyote sababu mdomo wangu ni wa mwanamke mmoja tu,” aliwahi kuiambia Closer Weekly.

Msimamo huo ulimpelekea kupoteza dili ya dola milioni moja alipogoma kupigana busu na mwigizaji Virginia Madsen kwenye uandaji wa filamu ya Scoundrels 2010.

Alichujwa na nafasi yake kupewa David James Elliot. Neal amekuwa kwenye ndoa na mkewe Ruve tangu 2003.

Kirk Cameron

Anao msimamo mkali kama wa Neal. Kwenye utengenezaji wa filamu ya Fireproof (2008), Kirk mwenye imani kali ya Kikristo aligoma kupigana busu na mwigizaji aliyevalia uhusika wa mkewe.

Japo kwenye filamu hiyo anaonekana akipigana busu, yule ni mke wake Noble Chelsea ambaye pia ni mwigizaji.

Baada yake kugoma, iliwalazimu maprodusa kumchukua Noble na kumpa uhusika huo kwa kumkarabati ili afanane na yule mwigizaji aliyekuwa akiigiza kama mkewe.

Baada ya kumwoa mkewe Noble aliyekutana naye kwenye uigizaji wa filamu ya Growing Pains, Kirk aliahidi kutomla denda mwanamke mwingine ambaye si mkewe.