Makala

Kilio cha mjane Mkenya anayeoza mguu Saudia Arabia

May 16th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

MJANE raia wa Kenya mwenye watoto watano aliyehusika kwenye ajali miezi mitatu iliyopita nchini Saudi Arabia na kulazwa katika hospitali moja ya Mashariki ya Kati bila matibabu sasa anaomba msaada.

Bi Margaret Ndanu Mutua, 43, alisema mguu wake unaoza na hawezi kupata matibabu kwa kukosa stakabadhi zilizokwamiliwa na mwajiri wake baada ya kuacha kazi.

Alisema juhudi za kupata msaada kutoka Ubalozi wa Kenya nchini Saudia, hazijazaa matunda, kwani hana stakabadhi za kuthibitisha uraia wake.

Alidai aliyekuwa mwajiri wake anazuilia nyaraka na stakabadhi zake muhimu na alizipoteza nyingine wakati wa ajali.

“Mguu wangu umeoza. Nimekuwa mzigo kwa watu. Nimejaribu hospitali zote bila mafanikio. Nahitaji matibabu ya dharura,” aliomba Serikali ya Kenya kuingilia kati kumsaidia kurejea humu nchini.

Katika kijiji cha Kalunga, eneo la Kaewa, Kaunti ya Machakos, anapotoka mama huyo, hali ni mbaya zaidi. Dada yake, Joyce Mutua, alifichua kuwa mwanawe wa pili, Bi Mutua amelazwa, katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kuchomeka na anahitaji Sh200,000 za matibabu.

Pia, babake Bi Ndanu anaugua.

“Tunaomba msaada ili aweze kurejea nchini. Nahofia huenda tukampoteza iwapo hatapata matibabu ya haraka,” alisema Bi Joyce.

Bi Ndanu anakumbuka akiamka akiwa na uchungu mwingi kutokana na mguu wake kuvunjika katika Hospitali ya Serikali ya King Suleiman, Januari 30, 2024.

Mama huyo aliondoka nchini Juni 26, 2021, kutafuta kazi katika nchi ya Uarabuni kama mjakazi kwa muda wa miaka miwili kulingana na mkataba.

Lakini alitoroka kutokana na mazingira mabaya ya kikazi.

Hospitali ilimfukuza kwa kukosa stakabadhi ambazo zingemwezesha kupata tiba baada ya mwajiri wake kukosa kulipa bili ya Sh31,287 kila mwezi ili kutimiza masharti ya mkataba wake.

“Niliwacha nyaraka zangu, ikiwemo pasipoti na kitambulisho. Mwajiri wangu alikataa kunipa. Nilikuwa na matumaini Ubalozi ungenirudisha nyumbani,” alieleza Bi Ndanu.

Baadhi ya Wakenya nchini Saudi Arabia huwakimbia waajiri wao na kuvunja kandarasi zao ili kutafuta ajira mpya bila kutumia wakala.

Ingawa mapato katika kazi ya aina hii ni bora, ni hatua hatari kwa sababu ikiwa lolote litatokea, mashirika ya awali ambayo yaliwapatia ajira hayawezi kuingilia kati, ambayo ni kesi ya Bi Ndanu.

Baada ya kutoroka, alianza kufanya kazi za kawaida za nyumbani katika mji mkuu wa Riyadh, Saudi Arabia.

Hospitali hiyo ilimfukuza baada ya kupata fahamu. Bi Ndanu aliishia kuishi mitaani ambako alikuwa akitegemea wasamaria wema kwa ajili ya kumchangia chakula, kabla ya msamaria mwema anayeishi naye kwa sasa kumchukua na kumpa malazi.

Pia, alisema Ubalozi wa Kenya ulimfukuza kwa kukosa stakabadhi ambazo zingemwezesha kujitambulisha kama Mkenya.

“Ubalozi haukunipa nafasi ya kujieleza. Mimi ni Mkenya, nazungumza lugha ya Kikamba na Kiswahili. Kakangu anaitwa Kasembi, Musyoka na dadangu anaitwa Joyce,” alisema.

Mama huyo alipata kazi katika taifa hilo la Uarabuni kwa hisani ya Mkenya “Job Majuu” na kampuni ya wakala ya Saudi Arabia’s Platinum.

Mkenya anayemsaidia Bi Ndanu, Bw Twalib Sunduli Nacheri, alisema alimpata mnamo Machi 27, 2024, katika hema la Kubera akiwa na uchungu mwingi huku akilia.

Alisema Ubalozi ulimweleza hauwezi kumrudisha nchini akiwa bado mgonjwa.