Habari za Kitaifa

Kinachofanya wavuvi kuangamia Ziwa Victoria

Na GEORGE ODIWUOR September 6th, 2024 2 min read

WAVUVI wengi wanaangamia wanapozama katika Ziwa Victoria kwa kukosa kuvalia jaketi za kuokoa maisha. Walinzi na wasimamizi wa  fuo wanasema wavuvi wengi wanapuuza sheria na kanuni za uvuvi na kuweka maisha yao kwenye hatari.

Katika kisa za Jumatano, Septemba 4, 2024 mvuvi mmoja Kaunti ya Homa Bay aliaga dunia baada ya kuteleza na kutumbukia ziwani.

Kulingana na Ngegu Caleb Okech, Mwenyekiti na msimamizi wa masuala ya uvuvi katika eneo hilo, Bw Willis Okech aliaga dunia kwa sababu hakuwa amevaa jaketi ya usalama walipokuwa kwenye shughuli zao za uvuvi.

Alisema sheria inawataka wavuvi wote kuvaa jaketi kila wanapokuwa ndani ya maji ili kupunguza hatari ya kuzama.

“Angekuwa hai kama angevaa jaketi ya usalama. Kwa bahati mbaya, hakuzingatia usalama,” Bw Okech alisema.

Okech alikuwa pamoja na wavuvi wengine katika mashua msiba ulipotokea.

Bw Fredrick Odhiambo, mmoja wa wavuvi waliokuwa pamoja na marehemu alisema Okech ndiye aliyekuwa akiendesha mashua hiyo na alikuwa ameketi pembeni.

“Alikuwa na jukumu la kudhibiti mwendo wa boti,” alisema Bw Odhiambo.

Bw Odhiambo aliripoti kuwa walikuwa wakijiandaa kutupa nyavu zao majini wakati ajali hiyo ilipotokea.

Alisema mwathiriwa aliteleza kutoka kwenye boti na kuanguka ndani ya maji.

“Bado hatuna uhakika jinsi alivyoanguka kutoka kwenye boti. Hata hivyo, hakuweza kuogelea kwa sababu ya mawimbi,” mvuvi huyo alisema.

Juhudi za wenzake kumuokoa hazikuzaa matunda.

Kulingana na Rais William Ruto, watu 5,000 hufa katika ajali Ziwa Victoria kila mwaka.

Akizungumza wakati wa mkutano mjini Kisumu wiki jana, Rais alisema serikali yake imejitolea kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuanzisha kituo cha uokoaji ambacho kitakuwa na wafanyikazi ambao watakabiliana na kisa chochote cha dhiki ziwani.

Katika Ziwa Victoria, kama vile barabarani, kuna idara zinazosimamia usalama ili wavuvi na watu wengine wanaotumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi wawe salama.

Mamlaka ya Bahari na Huduma za Walinzi wa Pwani ni miongoni mwa mashirika ya serikali yanayohusika na usalama katika ziwa hilo na yamekuwa yakifanya oparesheni kuhakikisha usalama wa wavuvi.