Habari za Kaunti

Kinaya mwanafunzi mwerevu anayezongwa na umaskini akiorodheshwa kwa wanaojiweza na Helb

Na SIAGO CECE August 21st, 2024 1 min read

MWANAFUNZI bora kutoka Kaunti ya Kwale amekumbwa na wasiwasi baada ya kuorodheshwa katika kundi la wanafunzi ambao familia zao zinajiweza katika mfumo mpya wa kufadhili elimu.

Licha ya Suheil Mumba kutafuta wafadhili wa kumsaidia kufikia ndoto yake ya kuwa daktari mwezi uliopita, hajafanikiwa kupata ufadhili kutoka kwa serikali kuu vile alivyodhania.

Suheil amewekwa katika daraja la tano (Band 5), ambalo kulingana na Wizara ya Elimu, ni la familia zinazopata kipato cha zaidi ya Sh120,000 kila mwezi.

SOMA PIA: Mwanafunzi bora wa KCSE Kwale akosa karo ya kusomea Udaktari

Kilichomshangaza ni kuwa wazazi wake wote hawajaajiriwa, na hufanya vibarua vidogo ili kujikimu kimaisha.

“Niliposikia kuwa barua mpya ya shue ilikuwa imetoka, nilifurahi nikitarajia kuwa serikali itagharamia karo yangu ya shule. Lakini sijaelewa kwa nini nimewekwa katika Band 5,” Suheil alisema katika mahojiano na Taifa Leo.

Alieleza kuwa ombi lake la awali la kutafua wafadhili halikufaulu, kwani watu wengi ambao wangemfadhili walisema serikali ina mpango wa kusaidia na kugharamia karo ya wanafunzi hasa waliotoka kwenye familia maskini kama yeye.

Hata hivyo, alipata usaidizi wa kugharamia chumba cha kulala katika Chuo kikuu cha Egerton, Kaunti ya Nakuru.

Suheil alikuwa mwanafunzi bora wa KCPE katika shule yake ya msingi baada ya kupata alama 389.