Makala

KINAYA: Wadau wa Mlimani hawatoshei katika mfuko wa yeyote yule

June 22nd, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

HII ni Kenya ya mwaka wa 2019, si ile ya 1969!

Hivyo? Unapotishia kuwasaga watu kwa sababu wamekupa changamoto kisiasa, kumbuka tuna Katiba ya 2010.

Nakuapia Jalali hata Mzee Jomo akifufuka leo, aikute Katiba hii isiyomdekeza kiongozi wa taifa kama ya zama zile, atalala tena. Milele!

Zama hizo Jomo aliitwa ‘mtukufu, baba wa taifa, mwanzilishi’ na kadhalika, sikwambii aliimbiwa na nyimbo nyingi tu za kumkweza na kumtukuza.

Nimesema hii si Kenya ya 1969 aliyotawala Jomo kwa maana zama hizo alimkalia mguu wa kausha makamu wake wa kwanza, ‘Dume’ Jaramogi Oginga.

Chama cha ‘Dume’ kilichojulikana kama Kenya People’s Union (KPU) kilifyekwa na kusombwa mbali kama magugu maharibifu, uchaguzi mdogo ukaandaliwa, waasisi wakahasiwa!

Mzee Jomo hakuwa na mfano wake, hatukujua yeyote wa rika lake, aliyesoma naye wala hatukuthubutu kuuliza walikokuwa watu hao ili tusimkasirishe.

Tulidhani ni mja wa kipekee, malaika mkali wa vita kama Mikaeli ambaye angempuliza mtu tu atoweke asionekane tena. Sasa mambo yamebadilika.

Leo hii mwanawe haitwi ‘baba wa taifa’ na mtu, hawezi kupiga marufuku chama chochote cha kisiasa, hateui majaji, havunji Bunge, hana bakora, ana sauti tu.

Anayo pia matusi ya hapa na pale, macho ya kutukodolea na kututishia, ila hayo tumezoea. Hayaui. Hayaumizi. Hayakondeshi. Haitupigi mishipa, yatatuacha hapa.

Matusi

Tumewahi kuitwa ‘mavi ya kuku’, tukaambiwa sisi ni ‘bure kabisa’, lakini aliyetutukana hivyo alituacha papa hapa na hatujaondoka.

Kabla ya kuitwa kinyesi cha kuku, ambacho kwa kweli hunuka vibaya mno, tulikaliwa mguu wa kausha na Mzee Kirungu kwa miaka 24 na akatuacha hapa tu.

Huyo naye ni mwingine! Siku zake chama cha Kanu kilikuwa ‘baba na mama’; ungekosana na mkeo nyuma ya pazia, akusingizie kutukana Kanu, utiwe ndani!

Huyo pia aliondoka, sikwambii watoto waliozaliwa alipochukua hatamu za uongozi washagonga miaka 40 na ushei, wengi wanaitwa baba, baadhi yao babu.

Huo ndio moyo wa Mkenya, chuma kizito na cha kudumu kilichohimili kutu, seuze kiumbe aliyeumbwa kama sisi, asiyeweza kutuumbua kwani hakutuumba?

Na hatuogopi yeyote wala chochote kwa sababu tunajua sheria inatulinda vilivyo, haki zetu za kujieleza na kufungamana na upande wowote kisiasa hazina ubishi.

Tusingekuwa na Katiba ya 2010 iliyo na haki za binadamu za kupigiwa mfano, Jomo mdogo angefanya anachoota kwani amemuoa kisiasa mtetezi wetu: ‘Baba’.

Mume wa mama yako, ajapokuwa mgumba, ni baba yako. Wakati mwingine mama hujiuma ulimi ili azuie kutoa ya moyoni, alinde ndoa yake. Tunaelewa.

Ukifuatilia yanayoandikwa mitandaoni tangu Jomo mdogo atishie kuwasaga waasi walio na asili ya Mlima Kenya, utajua Wakenya wote ni ‘wanaume’!

Hakuna anayeogopa, watu hawafichi majina yao, tena wanainukuu Katiba sawasawa na kurejelea historia yetu.

Sioni ajabu katika vitisho vya Jomo mdogo; amewatishia mafisadi, wangali nasi; alimtishia ‘Baba’ kabla ya kuapishwa kuwa ‘Rais wa wananchi’, sasa ni msiri wake.

Alitishia kuwarudia na adhabu ‘wakora’ waliobatilisha kuchaguliwa kwake kwa Agosti 2017, wangali wanachapa kazi zao kama kawaida.

Kwa ufupi, aendelee kututishia, nasi wazalendo tuendelee kufurahia haki zetu kama anayetuimbia ‘Mugithi’ wa Mike Rua uhanikizao hewani usiku wa manane.

[email protected]