Habari za Kitaifa

Kindiki atakiwa kusafisha jina kufuatia maafa ya Gen Z wakati wa maandamano 

Na SAM KIPLAGAT August 6th, 2024 2 min read

KUNDI la wapiganiaji wa haki za kibinadamu sasa wameelekea kortini kuzuia kuteuliwa tena kwa Profesa Kithure Kindiki na Aden Aduale na pia uteuzi wa Opiyo Wandayi kwenye Baraza la Mawaziri.

Wanachama 12 wa makundi hayo ya haki chini ya Muungano wa Kenya Bora Tuitakayo, wanasema uteuzi wa watatu hao unaenda kinyume na Katiba.

Kuhusu Profesa Kindiki ambaye aliteuliwa tena kama Waziri wa Usalama wa Ndani, wamesema uteuzi huo utavuruga uchunguzi ambao unaendelea dhidi ya maafisa wa usalama walioua raia wakati wa maandamano ya Gen Z.

Isitoshe, wanahoji uteuzi wa Profesa Kindiki utazima uchunguzi dhidi ya wahalifu wanaodaiwa kukodishwa na serikali kuwakabili waandamanaji na pia wahalifu wengine walioingilia maandamano miezi ya Juni na Julai, 2024.

Wakiongozwa na mwanaharakati Cyprian Nyamwamu, wamesema Tume ya Kitaifa Kutetea Haki za Kibinadamu kwenye ripoti yake mnamo Julai 24, 2024 ilisema watu 60 walifariki na wengine 666 bado walikuwa hawajapatikana.

“Ni ukiukaji wa sheria na ukosefu wa utu kwa Profesa Kithure Kindiki kurejeshwa katika wizara ya usalama ilhali kwa kipindi cha miezi 20 alioushikilia wadhifa huo, kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu,” akasema Bw Nyamwamu katika stakabadhi za kesi alizowasilisha.

Pia wanaharakati hao wamesema uteuzi wa Bw Wandayi unaangamiza demokrasia kwa kuwa alikuwa kiongozi wa wachache bungeni.

Hali kadhalika, wanaharakati hao walisema Rais Ruto alikiuka Katiba kwa kuteua Bw Duale, Bi Alice Wahome na Kipchumba Murkomen kama mawaziri mwanzoni mwa utawala wake ilhali wakati huo walikuwa wabunge.

Wanasema chaguzi ndogo ambazo ziliandaliwa katika maeneo ambapo wanasiasa hao walikuwa wakiwakilisha yaligharimu wapigakura pesa ambazo zingeelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Pia walisema uteuzi wa Bw Wandayi utasababisha mlipa ushuru agharimike kwa kuwa uchaguzi mdogo lazima utaandaliwa katika eneobunge alilokuwa akiliwakilisha la Ugunja.

Wanaharakati hao wamesema Profesa Kindiki ametajwa sana na anastahili kujukumika kutokana na visa vya watu kutokomea kwa njia ya kutatanisha, matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, kujeruhiwa kwa waandamanaji, kutekwa nyara na haki zao kukiukwa.

“Profesa Kindiki anastahili kurejeshwa katika baraza la mawaziri iwapo uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki unaomkabili utatamatika kisha apatikane hana hatia. Ni matumizi mabaya ya mamlaka kwa Rais kuwarejesha Duale na Kindiki katika baraza la mawaziri,” akasema Bw Nyamwamu.

Hasa alimkemea Profesa Kindiki kwa kutoomba msamaha au kujutia ukiukaji mkubwa wa haki za raia wakati ambapo alikuwa akipigwa msasa na kamati teule ya Bunge la Kitaifa.

“Mahakama hii inafaa kutoa amri kuwa Katiba ya Kenya ina mamlaka hata kuliko Rais na kuzima uteuzi wa Profesa Kindiki,” akasema wakili Kibe Mungai ambaye pia anawakilisha wanaharakati hao.

Wanaharakati hao 12 pia wanataka korti iamuru kura ya maamuzi ifanyike hapa nchini kubaini iwapo Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua wanastahili kusalia afisini.

Tafsiri: Cecil Odongo