Michezo

Kipyegon afuzu nusu-fainali ya 1,500m kwa kishindo

Na BERNARD ROTICH August 6th, 2024 1 min read

SIKU moja tu baada ya kuikosa nishani ya dhahabu kichupuchupu kwenye mbio za mita 5,000, Faith Kipyegon amerejea kwa kishindo na kufuzu kwa nusu-fainali ya mbio za mita 1,500.
Wakenya wengine waliofuzu kwa nusu-fainali hiyo itakayofanyika Alhamisi ni Susan Ejore na Nelly Chepchichir.
Fainali imepangwa kufanyika Ijumaa.
Kipyegon alimaliza katika nafasi ya nne katika mchujo wa pili ambao mshindi wake alikuwa Diribe Welteji wa Ethiopia aliyemaliza kwa muda wa 3:59.73.
Mwingereza Georgia Bell alitwaa nafasi ya pili mbele ya Nikki Hiltz wa Amerika aliyemaliza kwa muda wa 4:00.42.
Ejore alifuzu baada ya kumaliza kwa 3:59.01 katika nafasi ya tatu kwenye mchujo mwingine ambao mshindi alikuwa Gudaf Tsegay aliyemaliza katika muda wa 3:58.84, wakati Laura Muir wa Amerika akimaliza kwa muda wa 3:58.91.
Chepchichir alimaliza wa kwanza katika mchujo wa tatu kwa muda wa 4:02.67 mbele ya Jessica Hull wa Australia aliyemaliza kwa muda wa 4:02.70, wakati Elle St. Pierre wa Amerika akimaliza katika nafasi ya tatu kwa 4:03.22.