Habari za Kaunti

Kiwanda cha chuma cha Sh11 bilioni kuleta matumaini mapya Taita Taveta

Na LUCY MKANYIKA  August 5th, 2024 3 min read

SERIKALI inaharakisha ujenzi wa kiwanda cha chuma cha Sh11 bilioni katika Kaunti ya Taita Taveta kinachotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa eneo hilo lenye utajiri wa madini ya chuma.

Shughuli ya ujenzi imeratibiwa kuanza mwezi huu wa Agosti 2024.

Mnano Jumamosi, kampuni ya Devki Steel Mills ilikabidhiwa rasmi shamba la ekari 500 ili kuanza ujenzi wa kiwanda hicho katika eneo la Manga, kaunti ndogo ya Voi.

Kwa miaka mingi, wakazi wanaoishi karibu na eneo la Kishushe, ambako madini ya chuma yanachimbwa, wameishi katika umaskini mkubwa licha ya kuwa na madini mengi katika ardhi yao.

Kujengwa kwa kiwanda cha chuma ni ishara ya matumaini, kikitarajiwa kubadilisha maisha ya wenyeji kwa kubuni ajira, kuboresha miundombinu, na kukuza uchumi na biashara za eneo hilo.

Akizungumza wakati wa kukabidhiwa eneo hilo katika eneo hilo, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za Devki, Narendra Raval, alisema ujenzi wa kiwanda utaanza mara moja na utachukua miezi minane kukamilika.

KUTOKA KUSHOTO: Gavana Andrew Mwadime, Naibu Gavana Christine Kilalo na Katibu katika Wizara ya Madini Elijah Mwangi wakitoa hatimiliki mwigo ya ardhi kwa Mwenyekiti wa kampuni ya Devki Narendra Raval (pili kulia) na familia yake, itakayojengwa kiwanda cha kufua vyuma eneo la Manga mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Katika ziara yake katika kaunti hiyo wiki moja iliyopita, Rais William Ruto alisema atakuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Agosti.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa maelfu ya nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na hivyo kuleta matumaini kwa wenyeji wengi ambao wamekuwa wakihangaika kupata ajira.

Wakati wa awamu ya kwanza ya ujenzi, wakazi 3,000 wanatajiriwa kupata ajira huku zaidi ya 2,000 watapata ajira za moja kwa moja mara tu kiwanda kitakapoanza kufanya kazi.

Bw Raval alisema kuwa kampuni yake itasaidia wakazi kuingia katika uchimbaji wa madini ya chuma huku akitilia maanani wachimbaji wadogo wadogo ili wawe na uwezo wa kuuza madini hayo kwa kiwanda hicho.

“Nitasaidia jamii ya eneo hili kuchimba madini ili tuunde ajira na kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Nitashirikiana na serikali na nataka kuwahakikishia kuwa kiwanda hiki kitabadilisha maisha ya wakazi,” alisema.

Nchi inapojipanga kama kituo cha kimkakati cha usindikaji na kuongeza thamani kwa madini yake, serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuunda mazingira mazuri kwa wawekezaji kufaidika na vilevile wananchi.

Katibu wa Madini Elijah Mwangi alisema kwa kujitolea kwa serikali ya kitaifa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini, kuna matumaini kuwa mchango wake kwa Pato la Taifa utaongezeka kwa kiasi kikubwa, na hivyo kuongeza uchumi wa ndani.

“Sera ya serikali kuhusu kuongeza thamani itadumu katika maeneo ya uchimbaji madini. Tunataka kuongeza mchango wa Pato la Taifa kutoka asilimia moja hadi asilimia kumi,” alisema.

Migogoro ya uchimbaji madini

Gavana Andrew Mwadime alisema ujenzi wa kiwanda cha chuma katika eneo hilo unatoa fursa ya kipekee ya kuondoa umaskini ambao umeghubika jamii kwa miaka mingi.

“Mwekezaji yuko tayari kuwakaribisha wachimbaji wadogo wadogo. Atakuwa akikusanya madini ya chuma kutoka kwao kwa hivyo naamini kila mtu atafaidika,” alisema.

Hata hivyo, uchimbaji wa chuma umekuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa.

Eneo la Kishushe ambapo madini hayo huchimbwa imekumbwa na migogoro ya kisiasa na utata wa usimamizi haswa wa renchi ya Kishushe.

Shirika hilo limeondoa kibali chake kwa kampuni inayochimba madini hayo ya Samruddha Resources Kenya Limited na hivyo kupelekea kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako alitoa wito kwa serikali ya kaunti na serikali ya kitaifa kutatua masuala yanayozunguka uchimbaji wa madini ya chuma katika renchi ya Kishushe.

Aidha, aliwataka viongozi wa eneo hilo kuingilia kati ili kutatua migogoro hiyo haraka ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo hataathirika.

“Natoa wito kwa gavana kushughulikia mgogoro wa ardhi na usimamizi katika renchi ya Kishushe. Lazima tutatue mgogoro huo tunapojipanga kwa mradi huu mkubwa ambao utabadilisha maisha ya jamii ya eneo hilo,” alisema Mbunge Mwashako.

Kwa upande wake, mwekezaji Bw Mustapha Jamal, aliitaka serikali kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo.

“Kiwanda hiki kitakapokamilika, kitahitaji tani 100,000 kwa mwezi lakini kampuni ya Samruddha inaweza kutoa tani 10,000 pekee. Ikiwa tutaruhusu watu wengi zaidi basi jamii na serikali itafaidika,” alisema Bw Jamal.