Habari

Korti yasitisha uajiri wa Afisa Mkuu IEBC

June 22nd, 2019 2 min read

Na WALTER MENYA

MAHAKAMA ya Leba (ELRC), imesimamisha kwa muda shughuli ya kuwahoji watu wanaopania kujaza nafasi ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), iliyoratibiwa kuanza Jumamosi, hadi kesi iliyowasilishwa na kundi na mawakili itakaposikizwa na kuamuliwa.

Agizo hilo lilitolewa na Jaji Byram Ongaya ambaye sasa ameamuru kundi hilo linalojitambulisha kama Chama cha Mawakili, kukabidhi IEBC stakabadhi za kesi yao ili kutoa nafasi ya kusikilizwa kuanzia Jumatatu, siku ambayo mahojiano hayo yangeanza.

“Shughuli zote za kuwafanyia ukaguzi, kuajiri au kujaza nafasi ya Katibu na Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC zimesitishwa hadi kesi iliyowasilishwa na walalamishi isikizwe na kuamuliwa,” Jaji Ongaya sema.

Chama cha Mawakili, kupitia wakili Dkt Paul Ogendi, kiliwasilisha ombi la kusimamisha mahojiano hayo kwa sababu tume hiyo ilifeli kutoa kazi hiyo kwa kampuni ya wataalamu wa masuala ya wafanyakazi ili kuondoa tashwishi ya kuwepo kwa mapendeleo.

Pia walisema kuwa IEBC ilifeli kueleza ni kwa nini watu wengine waliorodheshwa kwa mahojiano na wengine wakaachwa.

Suala la vigezo vilivyotumika na tume hiyo kuandaa orodha hiyo ya watu 10 na wale walioendesha shughuli hiyo pia liliibuka katika kesi ya mawakili hao.

Kabla ya mawakili hao kwenda kortini kusimamisha mahojiano hayo, waliiandikia IEBC wakitaka habari kuhusu orodha ya watu wote waliotuma maombi, wale walioorodheshwa na orodha ya kampuni zote zilizokuwa zimetuma maombi ya kuendesha kazi ya uajiri.

Wataka nakala ya sera

Vilevile, mawakili hao walitaka nakala ya sera ya uajiri wa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC miongoni mwa mengine.

Kufikia wakati ambapo mawakili hao walikwenda kortini, IEBC haikuwa imejibu barua yao.

Tume hiyo ilikuwa imeorodhesha watu 10 kati ya 95 waliotuma barua za kuomba nafasi hiyo iliyosalia wazi mwaka jana baada ya Bw Ezra Chiloba kufutwa kazi.

Miongoni mwa walioorodheshwa ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) Dkt Joel Mabonga, Bw Hamprey Nakitari, Bw Zephania Aura, meneja wa IEBC katika kaunti ya Mombasa Nancy Kariuki, Bw Paul Kioko na Kaimu Afisa Mkuu wa IEBC Marjan Hussein Marjan.

Wengine ni Dkt Elishiba Murigi, Dkt Benjamin Tarus, Bi Anne Mwasi na Dkt Billow Khalid.