Habari

Korti yawaamuru maskwota kulipa bwanyenye Sh700,000

August 11th, 2020 2 min read

Na PHILIP MUYANGA

MASKWOTA walioshtakiwa kwa kuvamia kipande cha ardhi cha ukubwa wa ekari 30 kilicho katika Kaunti ya Kilifi, wameagizwa kulipa wamiliki wawili wa shamba hilo Sh700,000 kama fidia ya kulitwaa bila idhini.

Mahakama ya Mazingira na Ardhi pia ilitoa agizo la kutaka maskwota hao kubomoa na kuondoa nyumba na vibanda vyote walivyojenga katika ardhi hiyo iliyo eneo la Junju, kabla siku 90 zikamilike.

Agizo la mahakama ni kuwa, endapo maskwota hao hawatabomoa, basi wenye shamba hilo Bw Hamid Bin Mohamed na Bi Rukia Hemed ambao waliwasilisha kesi mahakamani watakuwa huru kuwafurusha.

Uamuzi huo wa Jaji James Olola ambao uliandikwa Julai 24, 2020, ukajulikana wikendi, uliamuru maskwota hao wasionekane katika shamba hilo kwa njia yoyote ile, baada ya kipindi hicho cha siku 90 kukamilika.

“Baada ya kutoa ushahidi ambao haukupingwa kuonyesha kuwa wao ndio wamiliki waliosajiliwa wa ardhi hiyo, imedhihirika walalamishi ndio wenye kipande cha ardhi na maskwota hawafai kuwa katika ardhi hiyo bila ruhusa yao,” alisema Jaji Olola.

Mahakama ilisema maskwota hao hawakupinga shtaka la kuwa wamejenga katika shamba la walalamishi bila ruhusa.

Jaji Olola alisema alikuwa ameridhika ya kuwa Bw Mohamed na Bi Hemed walikuwa wamethibitisha kesi yao.

Bw Mohamed na Bi Hemed waliiambia mahakama kuwa, licha ya kumiliki shamba hilo, maskwota wamekuwa wakilivamia tangu Machi 2014 na wamekuwa wakikata miti na kujenga mabanda kwa minajili ya kunyakua ardhi hiyo.

Waliiambia mahakama ya kuwa, walipoenda kukagua ardhi hiyo, baadhi ya viongozi wa eneo hilo walianza kuwaambia wakazi kuwa shamba hilo lilikuwa linagawanywa bila malipo, jambo lililofanya maskwota kuingia na kuanza kukata miti.

Kwa upande wao, maskwota hao walikanusha ya kuwa walalamishi ndio wamiliki wa shamba hilo huku wakisisitiza kuwa mababu zao walimiliki shamba hilo kwa zaidi ya miaka 100.

Kwingineko, Mahakama Kuu mjini Mombasa imetupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na wakazi wa mtaa wa Khadija unaomilikiwa na kaunti ya Mombasa wakipinga kuhamishwa.

Jaji Eric Ogola alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi lililowekwa na serikali ya kaunti.