Habari za Kitaifa

KTDA: Bonasi ya chai kulipwa kwa njia ya kidijitali

September 4th, 2024 2 min read

WAKULIMA wa majani chai nchini wakitarajiwa kuanza kupokea malipo yao ya bonasi mwezi ujao, Oktoba 2024, Shirika la Ustawi wa Majani Chai Nchini (KTDA), limewataka kufuatilia malipo hayo kwa mfumo wa kidijitali.

Mwenyekiti WA KTDA, Enos Njeru, anasema apu maalum ya simu ya mkononi kwa jina, “KTDA Farmers App” iliyozinduliwa na shirika hilo mwishoni mwa mwaka jana, 2024, inarahisisha upatikanaji wa maelezo kuhusu malipo kama hayo na mengineyo.

Aidha, wakulima wanapata habari sahihi kuhusu shughuli mbalimbali za KTDA.

“Tunawahimiza wakulima wetu kukumbatia matumizi ya teknolojia ya kisasa, kama vile apu maalum tulioanzisha katika kufuatilia maelezo ya huduma zetu, haswa malipo ya bonasi yatakayotolewa mwezi ujao wa Oktoba. Wakulima wetu wanazo simu za kisasa za mkononi na wanaweza kupata huduma hii kwa urahisi,” Bw Njeru, ambaye alihifadhi kiti chake katika uchaguzi wa mwezi jana, anaeleza.

Mkulima akielezea kuhusu kilimo cha majani chai. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, kupitia jukwaa hilo, wakulima wanaweza kupokea jumbe kila siku, kila wiki na kila mwezi kuhusu uzani wa majani chai yaliyowasilishwa viwandani.

Isitoshe, ndani ya “KTDA Farmers App” wakulima wanaweza kupata habari, maelezo na mafunzo kuhusu fani mbalimbali za kilimo cha majani chai kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa KTDA, anayesimamia kitengo cha Huduma za Usimamizi, Julius Onguso, majukwaa hayo ya kidijitali pia yatawawezesha wakulima kuagiza mbolea ya serikali ya bei nafuu.

“Kuzinduliwa kwa apu hii ni sehemu ya ajenda ya mabadiliko ya shirika hili ya kuliwezesha kuwahudumia wakulima kwa njia ya uwazi na wenye uwajibikaji. Ni matumaini yetu kwamba mfumo huu mpya wa utoaji huduma kidijitali utawafaidi pakubwa wakulima wetu hawa wenye mashamba madogo ambao ndio nguzo kuu katika sekta hii,” Bw Onguso anaeleza.

Wakulima wa majani chai wanatarajiwa kuanza kulipwa kupitia njia ya kidijitali. PICHA|SAMMY WAWERU

Apu hiyo inaweza kupakuliwa kupitia programu ya ‘Google Play Store‘ katika simu za kisasa zinazotumia Intaneti.

Imefanyiwa majaribio katika viwanda vinane vya majani chai nchini na kubainika kuwa bora zaidi.

Wakulima wa majani chai ambao hawana simu za kisasa wanaweza kutuma ujumbe mfupi kwa KTDA kupitia nambari 20213 ili kupata habari na maelezo wanayohitaji.

Aidha, wakulima wanaweza kutumia code ya USSD, *302# kuuliza maswali kuhusu uzani wa majani chai mabichi waliyowasilisha viwandani, hali ya malipo yao na uwepo wa mbolea.

Mkulima kama huyu anatarajiwa kunufaika kupitia KTDA Farmers App, mfumo wa kisasa kutoa malipo kwa wakulima wa majani chai nchini. PICHA|SAMMY WAWERU