Makala

Kutana na hakimu anayenunulia mahabusu boflo na maziwa washibe kwanza

April 14th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

PASCAL Eugene Nabwana ni hakimu ambaye amefanya kazi Kaunti ya Lamu kwa karibu miaka sita sasa.

Bw Nabwana, 40, anahudumu kama Hakimu Mkaazi Mwandamizi katika Mahakama ya Mpeketoni iliyoko Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi.

Utendakazi wa kipekee wa Bw Nabwana, ambao unazingatia sana haki na utu kwa washukiwa na hata mahabusu wenyewe wanaosukumwa magerezani umemwezesha kujizolea sifa kochokocho, hivyo kuibukia kupendwa na jamii nzima eneo hilo.

Miongoni mwa mambo yanayotofautisha utendakazi wa Bw Nabwana na mahakimu wengine nchini ni wakati ambapo mara nyingine utampata akiwanunulia wafungwa au washtakiwa waliofika mahakamani na kusubiri kwa muda mrefu kuitikia kesi zao boflo na maziwa ili kuwawezesha kushiba kwanza kabla ya zamu zao kufika kizimbani.

Anafanya mambo yote kwa kuzingatia itifaki, sheria na matakwa yote yanayofungamana na taaluma yake.

Anashikilia kuwa utu wake anaoonyesha kwa washukiwa au wafungwa haumaanishi kivyovyote vile atakaidi sheria kwa kuwahurumia wahusika anaowaonyesha utu huo wakati anaposhughulikia kesi zao wakiwa kizimbani mbele ya mahakama yake.

Bw Nabwana pia anatambulika kwa kuwa na upendo si haba hata kwa wale anaowahukumu kifungo gerezani-yaani mahabusu.

Kuna wakati moja ambapo alizuru gereza la kitaifa kaunti ya Lamu la Hindi GK Prison, ambapo baada ya masaa ya kuwapokeza makumi ya mahabusu ushauri wa kuwasaidia kubadili tabia zao na kuwa raia wema maishani wanapokamilisha vifungo vyao, Bw Nabwana alitoa Sh5000 za kuwanunulia mbuzi wafungwa hao ili wachinjwe na kuwawezesha ‘kupiga sherehe’ au wafurahie kama binadamu wengine kule nje.

Ni tukio ambalo liliteka nyoyo za mahabusu wengi, maafisa wa serikali, ikiwemo wakuu wa utawala na wanasheria wenzake aliokuwa ameandamana nao kwenye ziara hiyo ya jela ya Hindi kwa wakati huo.

Anatangamana na kila mwanajamii

Nabwana akiwa na Suparitenda Mkuu Wa Jela la Hindi, Bw Festo Odongo wakati wa ziara ya maafisa wa mahakama kwenye gereza hilo mnamo 2023. Picha|Kalume Kazungu

Ni kutokana na utu wa hakimu huyo ambao umemwezesha kutembea akiwa huru na kutangamana na kila mwanajamii mitaani, mara nyingi hata akiwa bila ya walinzi wake maalumu kama ifanyikavyo kwa mahakimu wengine Lamu na nchini.

Taifa Leo ilizama ndani kutaka kujua ni nini hasa kilimsukuma Bw Nabwana kufanya kazi ya hakimu kwa namna yake ambayo ni ya kipekee.

“Mnamo 2010, niliingia mjini Mombasa na kufanya kazi kwa miaka minane kama wakili niliyetetea washtakiwa mahakamani. Hapo ndipo nilipojifunza changamoto ambazo washukiwa hupitia. Ni hali iliyonifanya kuingiliana vyema na hata kuwajua washtakiwa kwa undani. Na ndio sababu nikimtazama mshtakiwa siwezi kudanganyika. Najua ni yupi mkweli na muongo,” akaeleza Bw Nabwana.

Anasema kufanya kazi ya kuamua kesi mahakamani siyo rahisi ila yeye amefaulu kuifanya kwa kuzingatia sheria na utu.

Anasema mara nyingi mahakimu hupitia kipindi kigumu maishani, hasa wanapoamua kesi zinazohusisha vifungo vikubwa, ikiwemo ubakaji, ugaidi, uuaji na nyinginezo.

“Unamuona mzee au babu akiwa na miaka karibu 70 na hapa unafaa kufuata sheria kikamilifu na kumfunga karibu miaka 30 gerezani kwa kosa la kubaka. Kwa upande mwingine unampata kijana wa miaka 20, ambaye ndiyo maisha anayaanza, akikabiliwa na kesi inayopaswa kisheria umfunge maisha. Yaani hapa unaona maisha ya mtu yakiharibika kabisa lakini kwa sababu tunafuata sheria, lazima jukumu ulitekeleze kikamilifu bila kuyumbayumba,” akasema Bw Nabwana.

Bw Nabwana aidha anawahimiza watu kuwa na mtazamo tofauti wa jinsi wanavyowachukulia wanaojipata pabaya kisheria.

“Watu wafahamu kuwa washtakiwa au wafungwa ni binadamu kama wao. Wajue kuna siku ambapo huenda walio huru pia wakajipata kwenye hali hiyo ya kuwa washtakiwa au mahabusu kwani katu sisi binadamu si wakamilifu. Tudumishe utu na kumuona kila mtu kuwa bora,” akasema Bw Nabwana.

Pia anawasihi watu kutafuta njia mbadala katika kutafuta haki, akishikilia kuwa siyo lazima kufuata mkondo wa kisheria mahakamani ila wanaweza kuongea na kusameheana, cha msingi kikiwa ni kuona jamii imepona na kuishi kwa umoja bila chuki.

Bw Nabwana alifichua kuwa kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu Lamu, wamekuwa wakizunguka sehemu mbalimbali za kaunti hiyo kuielimisha jamii kuibukia mazungumzo na utatuzi wa mizozo nje ya mahakama-yaani alternative dispute resolution (ADR).

Mkondo wa sheria kusuluhisha mizozo

Bw Nabwana akiwa Na Jaji Mkuu, Bi Martha Koome wakati wa ufunguzi wa kitengo maalumu cha kusuluhisha mizozo nje ya Mahakama kwenye korti ya Mpeketoni mnamo Aprili 18,2023. Picha|Kalume Kazungu

“Si lazima watu waegemee mkondo wa sheria ndipo wasuluhishe mizozo au tofauti zao. Kuna kuongea na kusameheana bila kufika kortini. Nahimiza sana mbinu hiyo kwani kufanya hivyo kwaleta ujirani mwema badala ya uadui au chuki miongoni mwa jamii. Pia kufanya hivyo hakuna gharama,” akasema Bw Nabwana.

Hakimu huyo aidha anaonya kuwa lazima jamii pia kufahamu kuna kesi zinazoruhusiwa kusuluhishwa kijamii kupitia kuongea na kusameheana nje ya korti ilhali nyingine zikiachiwa sheria kuchukua mkondo wake.

“Hapa si maanishi kesi zote watu waweza kuongea na kutatua nje ya korti kijamii. Lazima kutofautisha. Hatukubali kesi za ubakaji, ugaidi, wizi wa mabavu, unajisi, mauaji na zingine zozote za jinai kusuluhishwa kienyeji. Lazima hapa sheria iachiwe kutwaa mkondo wake kwenye kesi kama hizo,” akasema Bw Nabwana.

Bw Nabwana anatajiriba ya karibu miaka 14 sasa ya uanasheria.

Alifanya kazi kama wakili mjini Mombasa Kati ya mwaka 2010 na 2018.

Mnamo Novemba 2018, Bw Nabwana alipelekwa Lamu kama Hakimu Mkaazi wa Mahakama ya Mpeketoni, jukumu ambalo amekuwa akilitekeleza hadi sasa.