Makala

Mfanyabiashara azikwa, gari likiendelea kutafutwa mtoni Sagana

May 31st, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Mei 2, 2024, mfanyabiashara Samuel Kamau,42, aliripotiwa kutoweka na ikadadisiwa kwamba alikuwa ametumbukia ndani ya Mto Sagana akiwa na gari lake la kibinafsi.

Dokezi za polisi wa Kaunti ya Kirinyaga ziliashiria kwamba Kamau ambaye alikuwa ni baba wa watoto watatu, alikuwa akiongea na rafiki yake wa kutoka Kaunti ya Murang’a kwa njia ya simu na ambapo ghafla katika simu hiyo ya mwendo wa saa mbili usiku alitamka maneno “Mungu wangu, kwanza acha”.

Alisemwa kutamka maneno hayo akiwa karibu na mpaka wa kaunti za Murang’a na Kirinyaga katika barabara ya Murang’a-Sagana. Mto Sagana ndio mpaka wa kaunti hizo mbili na alisemwa kutumbukia ndani yake karibu na daraja la kuvuka hadi Kirinyaga.

Pia, aliposemwa kutumbukia kwa mto ni takriban mita 150 kutoka jengo la familia yao linalojulikana kama Chakaka ndani ya mipaka ya Kirinyaga.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi ya maafisa wa kituo cha polisi cha Kiamaciri kilichoko katika kaunti ndogo ya Ndia, Kamau alikuwa ameonekana mara ya mwisho katika eneo la burudani la Laibon Gardens lililoko Kaunti ya Murang’a kabla ya kuanza safari yake ya kurejea kauti ya Kirinyaga kwa gari lake.

Mnamo Mei 11, 2024, mwili wake ulitolewa ndani ya Mto Sagana katika hali ambayo hadi sasa haijawahi kueleweka vyema na marafiki wake wa karibu.

Hadi waleo, gari lake aina ya Nissan Navara lenye usajili KBT 171U halijawahi kuonekana huku maafisa wa uchunguzi wakidai kwamba bado liko ndani ya mto huo.

Maswali sasa yameanza kuibuka kuhusu jinsi uchunguzi huo uliendeshwa na mazingara hasa yaliyowafanya waliosema alitumbukia ndani ya mto huo kuamini hivyo.

“Mimi sitaki kuonekana kama aliye na mawazo ya kukera kuhusu mauti ya Kamau. Alikuwa rafiki yangu wa dhati na kuna yale ambayo tulikuwa tukiongea naye, mengine yakiwa ya usiri wa ndani. Kwa mfano, ndani ya familia yao aliniambia huwa na mzozo mkubwa wa mali na alikuwa akihofia kwamba uhasama huo ulikuwa ukionekana kuwa hata hatari kwa maisha ya waliokuwa hai ndani ya familia yao,” akasema Bw Stephen Njogu kutoka Kaunti ya Murang’a.

Alisema kwamba aliangalia ripoti ya uchunguzi kuhusu mauti ya Kamau lakini hakupata maelezo ya kumfanya aelewe kuhusu jinsi alivyoaga dunia.

“Uchunguzi wa polisi unafaa kuwa na uwazi na maelezo kamili ambayo yatasaidia wote walio na haja ya kujifahamisha na tukio walielewe kwa njia ya kisawasawa. Polisi wakisema Bw Kamau alitumbukia ndani ya mto, ripoti hiyo inafaa kuandamana na taarifa za aliyeshuhudia au walioshuhudia, tuoneshwe ushahidi wa hali ilivyokuwa wakati wa kutumbukia na hali zote za kumtafuta na kumpata akiwa ndani ya maji ziwe na uwazi wa kueleweka,” asema.

Ripoti ya uchunguzi inasema kwamba “kuna bawabu aliyekuwa karibu na mto huo ambaye aliona kitu kama mataa angani na kisha yakatumbukia ndani ya mto huo kwa kishindo na kulikuwa kukinyesha”.

Kando mwa mto huo hakukuwa na alama za magurudumu au ishara za fujo ambazo magari huzua yanapokataa udhibiti.

Katika hali hii, gari hilo likisemwa lilipaa angani umbali wa zaidi ya mita 20 kutoka kwa barabara na kutumbukia mtoni.

Hali inakanganya zaidi wakati maafisa wa jeshi waliofika kusaidia kumsaka Bw Kamau na gari lake ndani ya mto huo waliondoka baada ya siku tano wakisema kwamba hawakuwa wakiona kitu chochote cha kuwasaidia kutimiza lengo hilo.

Kwa kawaida, mtu akifa maji, mwili wake huwa unaelea baada ya siku tatu lakini huu wa Bw Kamau ulipatikana ukielea baada ya siku 10 na hadi sasa, gari lake bado halijapatikana.

“Wapiga mbizi wa kutoka mkahawa mwingine ulio karibu na mji wa sagana ndio walipata mwili huo ukiwa kilomita mbili kutoka kwenye gari lake lilisemwa lilitumbukia ndani ya mto,” ripoti hiyo ya uchunguzi yasema.

Vile maafisa wa jeshi walishindwa kuupata mwili huo lakini ukapatikana baadaye na wapiga mbizi wa kijijini ni swali ambalo limekuwa gumzo kuu katika Kaunti za Murang’a na Kirinyaga.

Hatimaye, mtaalamu wa harakati za uokozi katika viini vya maji Bw Stephen Oduor Agoa anasema kwamba “dereva akitumbukia ndani ya mto au baharini akiwa ndiye alikuwa kwa usukani huwa na ugumu wa kutoka nje kutokana na mshtuko, uhaba wa hewa na mwangaza”.

Alisema kwamba “katika hali hii ya Kamau, kuna uwezekano kwamba ikiwa alitumbukia ndani ya mto huo na akaishia kuonekana akiwa nje ya gari lake, basi hakuwa amefunga madirisha ya gari lake na kabla ya lizame, alijaribu kujinusuru kwa kutoka nje na akaingia kwa maji na ndipo naye akazama”.

Bw Agoa alisema kinyume na hilo ni kwamba “basi kuna mtu anahadaa mwingine katika kisa hicho ikizingatiwa kwamba hata baada ya mvua ya mafuriko kutamatika kwa muda sasa gari lake bado halijaonekana ndani ya kipindi cha siku zaidi ya 20 sasa”.

Tayari alishazikwa katika kijiji cha Kiandai.

Alisema kwamba uchunguzi unaojaribu kutoa maelezo kuhusu hali hizo tata hasa hali ya kikosi cha wapiga mbizi cha jeshi la nchi kulemewa kuutwaa mwili lakini makurutu wakaweza ni baadhi ya masuala yanayozua shaka kuu.

Kwa mujibu wa Mzee Ndegwa Kiburi kutoka eneobunge la Kangema, babake marehemu akifahamika kwa jina Charles Kagwanja Kamau, alijipa umaarufu na ukwasi kupitia biashara ya kuuza chipsi katika jiji la Nairobi miaka ya 1970.

“Alianza kuwekeza faida yake katika miji mbalimbali ya kaunti za Nairobi, Kiambu na Kirinyaga lakini akaingia kwa ndoa ya wake wengi na ndipo masaibu ya familia yake yalianzia. Sisemi kwamba ndoa za aina hiyo ni mbaya kwa sababu zipo nyingi zilizofaulu,” asema.

Anasema kwamba waliomjua Bw Kagwanja walisononeka sana kuyapata mazingira ambayo aliaga dunia akiwa ndani yamo na hatimaye himaya yake ya uwekezaji ikaingiwa na ung’ang’aniaji ulioshia hata kijana mwingine wake kuaga dunia katika hali ya kutatanisha.

“Lakini yakifika ni masuala ya kutoa habari rasmi kuhusu mauti, ni maafisa wa polisi ambao hadi sasa hawajatupa habari za kuridhisha kuhusu mauti haya yanayosemwa yalitokea ndani ya Mto Sagana. Kabla ya maelezo hayo kutolewa, mtatuwia radhi kwamba ni lazima tujaribu kujipa ukweli wetu na ambao unaashiria kuna uzembe au utepetevu wa kuchunguza kiini kamili cha mauti hayo,” asema Mzee Kiburi.