Habari za Kaunti

KWS Murang’a bado kudhibiti tumbiri waharibifu

June 7th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

AGIZO la Rais William Ruto la mnamo Mei 10, 2024, kwa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) kwamba ianze harakati za kuwasaka tumbiri wanaokisiwa kuwa 100,000 na wanaotesa wakulima katika Kaunti ya Murang’a kwa kuharibu mimea na mavuno, halijaanza kutekelezwa.

Rais Ruto alitoa amri hiyo ya hadharani akiwa katika eneo bunge la Maragua alipojitokeza kushirikisha hafla ya upanzi wa miti katika msitu wa Kawaharura baada ya wenyeji kumweleza kwa sauti za juu kwamba harakati zao za kilimo zilikuwa zimekwamizwa na tumbiri hao.

“Nimesikia wananchi na mbunge wao (Bi Mary wa Maua) wamesema kwamba hawa tumbiri ni balaa kubwa kwa harakati zao za kilimo. Mkurugenzi wa KWS hapa amepata hiyo habari na anafaa aanze harakati za kuwasaka na kuwadhibiti,” akasema Dkt Ruto.

Lakini hadi sasa ambapo ni mwezi mzima unaelekea kuisha, hali ni ile ile huku kukiwa hakumna hata mtego mmoja wa kunasa wanyama hao umewekwa katika mashamba ya eneo hilo.

Badala yake, tumbiri hao wanazidi kuwa kero kuu kwa wenyeji, huku ikikadiriwa kwamba kwa siku moja pekee, wanyama hao hutuza Kaunti hiyo hasara isiyopungua Sh10 milioni.

“Hasara hiyo inakadiriwa kwa hesabu kwamba tumbiri mmoja ako na uwezo wa kuharibu mimea na mavuno ya Sh100 kwa siku. Hiyo ni hasara ya takriban Sh300 milioni kwa mwezi na ikiwa ni Sh3.6bilioni kwa mwaka. Ili kuhepa hasara ya aina hiyo, wengi wa wakulima wameachana na mambo ya kilimo hivyo basi kutwika kaunti nzima umasikini,” akasema mwenyekiti wa muungano wa wakulima wadogowadogo ukanda wa Mlima Kenya,  Bw James Kariuki.

Bw Kariuki alisema kwamba “nilipomsikia Rais Ruto ametoa amri kwa KWS kwamba wanyama hao wathibitiwe, wakulima walipata msisimko mkuu na inaonekana sasa kwamba amri hiyo ilikuwa tu mzaha na sarakasi kwa kuwa hakuna hata mikakati imezinduliwa ya kuwaandama tumbiri hao”.

Alisema wanyama hao huharibu mimea aina ya mboga na matunda, mihogo, viazi na nduma huku hata wengine wakivamia boma za watu “na kukama ng’ombe pamoja na kutoa mayai kutoka vyumba vya kuku”.

Mkurugenzi wa KWS katika kaunti hiyo Bw Laurence Kariuki alikataa kujibu suali la ni kwa nini amri ya Rais haijaanza kutekelezwa huku wakulima wakiendelea kupata hasara na kaunti kutumbukia katika hali ya umaskini.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaungama kuwa huenda Rais Ruto alitoa amri hiyo ili kuwafurahisha wenyeji waliokuwa wakimsikiliza akijua vyema kwamba huenda utekelezaji uwe na shida kwa kuwa tumbiri hao wamesambaa katika Kaunti zote ndogo tisa za Kaunti ya Murang’a.

“Mimi nilimsikiliza Rais vizuri sana akitoa amri hiyo na nikapata msukumo wa kutaka kuwachekelea wenyeji wa eneo hilo… Nilishindwa kuelewa jinsi wanyama hao wangeondolewa mashambani kwa kuwa kuanzia mwaka wa 2010 kilio kimekuwa ni hicho. Wanyama hao wamekuwa wakiongezeka kwa miaka hiyo 14 sasa na hata utawala wa Gavana wa kwanza wa Murang’a, Bw Mwangi wa Iria (2013 hadi 2022) ulikuwa ukijaribu hata kuwapa wakulima mitego lakini hakuna afueni iliyopatikana,” akasema mshirikishi wa masuala ya vijana katika eneobunge la Maragua, Bw Warui Gitau.

Bw Gitau alisema kwamba alichukulia amri ya rais kama mzaha wa kisiasa na akilenga tu kubakia na umaarufu wa hadaa kupitia kupitisha shida hiyo kutoka kwake hadi kwa KWS.

“Ikiwa rais alimaanisha amri yake itekelezwe anafaa airudie tena akiwa Jijini Nairobi akiuliza ni kwa nini shida hiyo bado iko Murang’a licha yake kutoa mwelekeo wa hadharani,” akasema.

Tumbiri hao wamekuwa wakizaana kwa kasi na inakisiwa kwamba kabla ya mwaka wa 2030 wakulima huenda wawe wakipanda tu miti au nyasi ambayo ndio tu mimea ambayo tumbiri hao huwa hawaharibu.

Kamishna wa Kaunti hiyo Bw Joshua Nkanatha alidinda kutoa neno lake kuhusu hali ilivyo kwa sasa licha ya kwamba yeye ndiye mshirikishi wa sera za serikali na macho ya Rais katika Kaunti ya Murang’a.

Bw Joseph Ndambuki akiwa shambani mwake. Alilia kwamba uharibifu wa tumbiri shambani mwake umesababisha hasara kubwa. PICHA | MWANGI MUIRURI