Habari za Kitaifa

Maafisa 5 wafikishwa kortini kufuatia kutoroka kwa mahabusu seli

Na RICHARD MUNGUTI August 21st, 2024 1 min read

MAAFISA watano kati ya nane waliohusishwa na kutoroka kwa washukiwa 13 kutoka kituo cha polisi cha Gigiri, Nairobi mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024 wamefikishwa katika Mahakama ya Milimani.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeomba Hakimu Mkuu Mwandamizi Martha Nanzushi awape idhini ya kuwazuilia kwa siku 14 ili uchunguzi ukamilishwe.

Hakimu ameambiwa kuwa wapelelezi wanataka muda huo kuwazuilia Koplo Ronald Babo, Konstebo Evan Kipkirui, Konstebo Millicent Achieng, Konstebo Zachary Nyabuto na Konstebo Gerald Mutuku ili wakamilishe uchunguzi kuhusu kisa hicho kabla ya kuwafungulia mashtaka maafisa hao.

Maafisa hao walikuwa zamu usiku wakati mahabusu 13 akiwemo mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 ambao mili yao ilipatikana katika timbo mtaani Kware, Embakasi walitoroka kutoka seli.

Collins Jumaisi Khalusha, aliyedaiwa kukiri kuwaua wanawake 42 lakini baadaye idadi ikapunguzwa hadi sita alitarajiwa kujibu mashtaka Ijumaa, Agosti 23, 2024.

Mahabusu wengine 12 walikuwa raia wa Ethiopia waliopatikana nchini kinyume cha sheria.

Usiku wa kisa, Koplo Babo alikuwa msimamizi, Konstebo Kipkirui alikuwa mlinzi wa seli na mwenzake Mutuku alikuwa katika ofisi ya kupokea ripoti.

Achieng na Nyabuto walikuwa zamu kulinda kituo hicho cha polisi.

Wapelelezi wa DCI wanaochunguza kesi hiyo waliambia mahakama walitaka muda wa kukagua simu za washukiwa na video za CCTV ambazo zilipelekwa kwa kitengo cha uhalifu wa mtandao.

Waliomba washukiwa wazuiliwe katika vituo vya polisi vya

Spring Valley, Parklands na Runda.

Hakimu Nanzushi atatoa uamuzi Alhamisi, Agosti 22, 2024.