Habari Mseto

Maafisa wa kliniki waendelea na mgomo ‘hadi kieleweke’

May 28th, 2024 2 min read

NA WACHIRA MWANGI

MWENYEKITI wa Maafisa wa Kliniki Nchini, Bw Peterson Wachira, amewaongoza wataalamu hao kutoka kaunti za Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Lamu, na Mombasa katika maandamano jijini Mombasa huku wakidai haki na heshima katika kazi yao.

Bw Wachira alisisitiza kuwa mgomo huo uliotimia siku 58 tangu Aprili 1, 2024, ulitokana na uzembe wa waajiri wao wa kaunti na kitaifa.

“Hata baada ya amri ya mahakama, waajiri hawakuheshimu amri hiyo, na hivyo kutulazimu kuendelea na mgomo,” Bw Wachira alisema.

Bw Wachira alionyesha kukosekana kwa nia njema ya kutatua mgogoro huu, akifafanua kuwa Bunge liliidhinisha bilioni Sh8 kwa ajili ya kuajiri walimu wa shule za sekondari msingi (JSS) katika mikataba ya kudumu (PnP), lakini ombi lao la Sh3.5bilioni kwa ajili ya kuweka waliokuwa kwenye kandarasi ya UHC kwenye mikataba ya kudumu limepuuzwa.

“Je, sisi si wananchi wa Kenya?” Aliuliza Bw Wachira huku akisisitiza kuwa maafisa tabibu walioko kwenye kandarasi ni lazima wawekwe kwenye mikataba ya kudumu (PnP) ili kuwe na usawa na haki kazini.

Bw Wachira alikemea hatua ya kupunguza mishahara wa maafisa wa kliniki walioko masomoni kutoka Sh115,000 hadi Sh50,000.

Alieleza kuwa wao ni wataalamu waliohitimu kama matabibu wengine na wanahitaji kupata ujuzi kazini bila kubaguliwa.

Aidha, alidai kuwa marupurupu ya hatari za kiafya yanafaa kuongezwa kutoka Sh3,000 hadi Sh15,000 kama walivyokubaliana mwaka 2021.

“Tuko hapa kutafuta heshima kwa kazi tunayoifanya. Katiba imesema kuwa hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa,” alisema Bw Wachira.

Katika matakwa 10 waliyoainisha mwanzoni mwa mgomo, Bw Wachira alisema kuwa wamekubaliana na saba kati ya hayo, na kubaki matatu pekee.

Alisisitiza kuwa hawatalegeza kamba hata kama mgomo utachukua siku 100 hadi 150.

“Lazima tuheshimiane na tuwe na haki kazini,” alisema.

Bw Wachira akikemea vitisho kutoka kwa Bodi ya Kuajiri ya Kaunti ya Mombasa, akisema kuwa mgomo wao ni halali kisheria na “hakutakiwi kuwa na vitisho vya kusimamisha mishahara ya maafisa wa kliniki”.

Aliwasihi maafisa wa kliniki wasirejee kazini hadi pale makubaliano ya kurejea kazini yatakapoafikiwa.

Maafisa wa kliniki wa kutoka Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Lamu, na Mombasa, chini ya muungano wao wa (KUCO), waandamana nje ya ofisi ya Gavana wa Mombasa mnamo Mei 28, 2024. PICHA | WACHIRA MWANGI