Habari za Kitaifa

Mackenzie kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla kushtakiwa kwa mauaji

January 17th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

MAHAKAMA Kuu ya Malindi katika Kaunti ya Kilifi imeagiza mshukiwa mkuu Paul Mackenzie kufanyiwa uchunguzi wa akili pamoja na washirika wake wanaohusishwa na vifo tata vya watu katika msitu wa Shakahola.

Mackenzie na washukiwa wengine 30 walifikishwa mbele ya Jaji Mugure Thande aliyetoa agizo hilo kabla ya kesi ya mauaji dhidi yao kusikilizwa.

Mackenzie na wenzake 30 wanakabiliwa na mashtaka zaidi ya 190 ya mauaji.

Akitoa agizo hilo, jaji Thande alisema Jumatano kwamba ukaguzi wa akili unafaa kufanyika kwa siku 14 kwa mujibu wa ombi la upande wa mashtaka na kuongeza kuwa washukiwa hao watafanyiwa uchunguzi huo kwenye miji mbalimbali iliyo karibu na sehemu ambazo wamezuiliwa.

Kulingana na jaji huyo ambaye amepinga ombi la mawakili wa mshukiwa wa kwanza–Paul Mackenzie–ambao awali walikuwa wamependekeza kupunguzwa kwa siku hizo hadi saba, amesema muda wa siku 14 utasaidia upande wa mashtaka kuendeleza shughuli za kusikilizwa kwa baadhi ya mashtaka ambayo yanamkabili Mackenzie na wafuasi wake kwenye mahakama mbalimbali zilizoko ukanda wa Pwani.

Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Februari 6, 2024

Kwa upande wao, naibu kiongozi wa mashtaka Victor Mule na mwenzake Victor Owiti, walielezea kuwa Mackenzie atawasilishwa kwenye mahakama ya Mombasa mnamo Alhamisi na pia kwenye mahakama ya Tononoka mnamo Januari 22, 2024.