Makala

Madereva wa malori ya trela wadai huona mizuka barabarani

January 12th, 2024 2 min read

NA RICHARD MAOSI

MADEREVA wa malori ya matrela katika barabara ya Nairobi-Mombasa wamedai kwamba mara kwa mara wao huona mizuka na vitu vingine vya kiajabu wanapokuwa safarini.

Matukio hayo mara nyingi hutokea usiku.
Igawa hii si mara ya kwanza kwa visa kama hivi kuripotiwa, siku za karibuni baadhi ya madereva wameingia kwenye mitandao ya kijamii kusimulia jinsi ambavyo visa vya kutisha wanapokuwa wakisafirisha mizigo, vinawaathiri.

Ni madai ambayo vilevile yameripotiwa katika barabara ya Eldoret-Nakuru, Msitu wa Malava, Kibwezi, Mbuinzau, Makindu, Kiboko na eneo la Sabaki katika barabara ya Malindi-Lamu.

“Mimi niliona kitu kama mwanadamu nilipokuwa nikitoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alikuwa katikati ya barabara akivuka polepole ikabidi nisimame mpaka apite ndipo niendelee na safari,” akadai Claudi Juakali.

Kulingana na Claudi, hangeweza kushuka usiku huo kwa sababu tukio lenyewe lilifanyika karibu na Mbuga ya Wanyama ya Tsavo, hivyo basi ilibidi asimame mbali mpaka ‘mzee wa watu’ alipopotelea msituni. Hatimaye Claudi akaendelea na safari.

Naye dereva mwingine, Bw Edwin Oseko, anasema alianza kutembea na mifupa ya nguruwe–kwa kuelekezwa kitamaduni–akiamini itamkinga dhidi ya viumbe wa ajabu usiku.

siku moja marafiki zake walimpa tahadhari wakimtaka awe macho kila mara anapokaribia eneo la Manyani karibu na Voi kwani “hapa husikika sauti za wanawake wakipiga stori ila huwaoni”.

Anasema ingawa sehemu hii huwa imewekewa ulinzi mkali kwa sababu ya ukaribu wake na Mbuga ya Tsavo, siku moja akiwa kwa gari, macho yake yalikutana na msichana mrembo akiwa amesimama kando ya barabara.

“Alinipungia mkono akitaka nisimame ila nilikanyaga mafuta bila kuangalia nyuma na kuanzia siku hiyo sijawahi kusimama labda ninapofika kwenye kituo cha kibiashara ambacho ninakifahamu kama vile Salgaa au Kikopey,” akasema Bw Oseko.

Lakini naye Bw Ndungu Joseph anasema baadhi ya madereva wamekuwa wakizabwa makofi au kuona vivuli vya wanawake ambao huwa hawaonekani hasa katikati ya misitu ya miti mirefu.

‘Mara nyingi huwa tunaishiwa nguvu kiasi kwamba hatuwezi kupiga picha matukio ya kutisha kama haya kwa sababu ya woga na mara nyingi viumbe wenyewe huwa na tabia ya kupotea,” akasema.

Hata hivyo Naomi Boyani ana wazo tofauti kwa sababu anasema dereva akianza kuona vitu kama hivi barabarani, ni ishara kwamba amechoka na hivyo basi anatakiwa kupumzika.

Anawataka madereva kupunguza miraa wanayotafuna kwa sababu huwapatia maruerue.

Mchungaji Millicent Obonyo kutoka eneo la Syokimau, anasema japo kuna nguvu za giza, muumini hana budi kupigana vita vya kiroho.
Bi Obonyo anasema binadamu anahitaji nguvu za ziada kutoka kwa Muumba ili kushinda mambo yasiyokuwa ya kawaida ambayo aghalabu huonekana katika ulimwengu wa kawaida.