Makala

Maimamu waunga mazungumzo, wajiondoa kwenye kesi dhidi ya Ruto, Gachagua

Na CECIL ODONGO July 29th, 2024 1 min read

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) sasa linaunga mkono mazungumzo kuhusu masuala ambayo yameibuliwa na Gen Z ili kukomesha zogo la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa  nchini.

Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado, jana alisema kuwa baraza hilo linataka muafaka wa kisiasa uafikiwe ili kuyashughulikia baadhi ya matatizo ambayo yameibuliwa na Gen Z wakati wa maandamano yao.

“Maandamano ya Gen Z yameweka wazi kuwa kuna masuala ambayo yanahitaji utatuzi nchini. Nchi inastahili kuanzisha mazungumzo hayo ili masuala ambayo yaliibuliwa na Gen Z yashughulikiwe kwa ukamilifu,” akasema Bw Ole Naado.

Alikuwa akiongea katika makao makuu ya Supkem katikati mwa jiji la Nairobi ambapo pia alisema kuwa nchi inaweza kusonga mbele tu kama Gen Z na serikali wataafikiana,

Wakati huo huo, Supkem imejiondoa katika kesi ambayo ililenga kuwaondoa mamlakani Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Kesi hiyo iliwasilishwa na mwanaharakati Cyprian Nyamwamu, Khelef Khalifa, Janet Muthoni, Paul Rukaria, Fred Ogolla na wengine sita.

Kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa Alhamisi wiki jana, wahusika waliwataka Rais Ruto na Bw Gachagua wajiondoe mamlakani kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa uongozi bora kwa Wakenya tangu wachaguliwe mnamo 2022.

Walisema kuwa uongozi wa nchi nao pia umekiuka katiba huku wakitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) iamrishwe na mahakama kuandaa kura ya maamuzi.

Kura hiyo inastahili kuandaliwa kuamua iwapo rais na naibu wake wanaweza kuondolewa mamlakani kwa msingi wa kukiuka katiba, kutumia mamlaka yao vibaya na kupoteza imani ya umma.

Walisema kuwa Rais na naibu wake walikuwa wamekiuka katiba mara 31 hasa kupitia kuwaongezea Wakenya ushuru maradufu, kuamrisha waandamanaji wauawe, waandamanaji kutokomea katika njia ya kutatanisha, kupanda kwa gharama ya maisha na serikalio kutiwa saini kwa mikataba ya kibiashara na Amerika.