Kindiki asuka mbinu kali kukwepa makosa ya Gachagua
NAIBU wa Rais, Prof Kithure Kindiki anaonekana kuchukua hatua za kimakusudi kuepuka makosa ya mtangulizi wake Rigathi Gachagua kwa kuhepa hafla za umma zinazohudhuriwa na Rais William Ruto tangu aapishwe kuwa naibu wa rais wa tatu wa Kenya.
Tofauti na mtangulizi wake aliyeonekana katika takriban hafla zote za Rais, Prof Kindiki anaonekana kufuata mwelekeo tofauti wa kuepuka mienendo iliyochangia naibu wa pili wa rais kutemwa.
Kwa mfano, tangu aingie enzini Novemba 1, Naibu Rais ameandamana na Rais katika hafla moja tu ya umma; kutawazwa kwa askofu wa Kanisa Katoliki la Embu, Peter Kimani.
Wachanganuzi wa siasa wanahusisha mtindo wa Prof Kindiki na weledi wa kutojisawiri kama rais mdogo alivyokuwa akifanya Gachagua.
Wanamwainisha Prof Kindiki kama chombo cha umoja na mshikamano wa kitaifa, utawala wa sheria, msaidizi mkuu wa Rais wala si kisawe chake, kiongozi wa kitaifa na kiungo cha demokrasia, mtaratibu, mwanadiplomasia na mtumishi bora wa umma .
“Ni weledi na hekima ambayo imemfanya kuwa na ratiba yake tofauti na Rais na kuepuka makosa ya Gachagua aliyejitokeza kama mwenza wa Ruto serikalini,” asema mdadisi wa siasa Paul Wafula.
Tofauti na Gachagua, anasema, Prof Kindiki amekuwa mstari wa mbele kupigia debe miradi ya serikali katika hafla zake.
“Tumemsikia akitetea mfumo wa afya wa SHA, akihubiri amani badala ya ukabila na kudhihirisha heshima kwa asasi za umma ikiwemo mahakama ambayo Gachagua alikuwa akishambulia,” asema .
Naye mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema ni wazi kuwa Prof Kindiki hajaonekana mara kwa mara pamoja na Rais Ruto kwenye hafla za umma kwa makusudi ya kimkakati.
“Ingawa Gachagua alihusika zaidi katika shughuli za umma na kisiasa za Ruto, mara nyingi akiandamana naye katika hafla kuu na kuonekana sana kwenye vyombo vya habari, pia hii ilimweka kwenye darubini, jambo ambalo Prof huenda analenga kuliepuka,” asema Dkt Gichuki.
“Pia kuna uwezekano kwamba nguvu ya Prof Kindiki iko kwingineko hasa kuchora mkakati wa kurekebisha makosa ya serikali,” anasema akitaja mifano kama vile wiki jana alipoahidi kuwa serikali haitaingilia utendakazi wa mahakama na kuhimiza majaji kuharakisha kesi mbalimbali.
“Tunahitaji kujalizana bila kuingilia uhuru wa mwingine. Sharti sisi kama taasisi za serikali tutafute njia za kushirikiana na kusaidiana ili kutimiza maono ya kila mmoja. Bunge litekeleze jukumu lake, serikali tawala itekeleze wajibu wake nayo idara ya mahakama itusaidie bila kuwa kizuizi,” akasema Pro Kindiki majuzi.
Aidha, Prof Kindiki, katika kikao cha Chama cha Wahariri Kenya (KEG) katika Kaunti ya Nakuru majuzi, alionesha majuto akiahidi kuwa serikali italipa deni lake kwa vyombo vya habari na kupanua wigo wa uhuru wa wanahabari nchini kinyume na hali ilivyokuwa chini ya Bw Gachagua kama naibu wa rais.
Dkt Gichuki anaongeza kuwa Bw Gachagua alikuwa amechukua nafasi kubwa katika kuendeleza ajenda yake ya kisiasa, mara nyingi akihudhuria mikutano kwa madhumuni ya kushughulikia masuala ya kibinafsi ya kisiasa.
Vilevile, anasema kuna uwezekano kuwa Prof Kindiki ametwikwa majukumu mengine na bosi wake, au amechagua kuhepa hafla za Rais kwa sababu za kibinafsi kuepuka makosa yaliyosababisha uhasama kati ya Bw Gachagua na Dkt Ruto.
Dkt Gichuki anaongeza: “Gachagua na Kindiki wanatoka katika asili tofauti za kisiasa, na hii inaweza pia kuakisi mienendo ya ndani ya muungano tawala wa Kenya Kwanza.
“Bw Gachagua, pamoja na ufasaha wake wa kuzungumza, mara nyingi alilandana kisiasa na Ruto na uwepo wake kwenye hafla za umma ulimsaidia Ruto kuimarisha uungwaji wake katika Mlima Kenya lakini pia ulisababisha mzozo wao.”
Tom Maosa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa naye anasema mkakati mkuu wa Prof Kindiki ni kuepuka kuonekana kama mshindani wa Rais Ruto. “Hii inaweza kueleza kwa nini haonekani mara kwa mara kwenye mikutano ya hadhara inayohudhuriwa na bosi wake,” anasema.
Bw Maosa anasema, Gachagua alikuwa amejipanga kimkakati ndani ya serikali, akishiriki mara kwa mara katika mahojiano na wanahabari, hotuba za hadhara na kuhudhuria hafla mbalimbali pamoja na Rais Ruto kama sehemu ya mkakati wake wa kisiasa kudumisha umaarufu kwa umma, hasa miongoni mwa wapigakura wa Mlima Kenya.
“Lakini kutoonekana kwa Kindiki katika mikutano ya hadhara ya Rais kunaweza kuwa kwa kimakusudi, pengine kuepuka mzozo na Rais Ruto.Bw Gachagua alishutumiwa kwa makosa kadhaa ambayo hatimaye yalichangia kung’atuliwa kwake.
Alilaumiwa kwa kusema kuwa Kenya ni kama kampuni iliyo na wenye hisa.Pia alishutumiwa kwa kumtishia Jaji Esther Maina aliyeshughulikia kesi yake ya ufisadi na kuonekana kumpinga Rais katika baadhi ya hafla.