Oyamo ajaribu kujinasua na mauaji ya Sharon
ALIYEKUWA msaidizi wa Gavana wa zamani wa Migori Okoth Obado amejaribu juu chini kujinasua na madai kwamba alimsaliti Sharon Otieno na kumkabidhi kwa majambazi waliomuua baada ya kumbaka ndani ya msitu usiku wa Septemba 3,2018.
Sharon Otieno, aliyekuwa mwanachuo alikuwa ametundikwa mimba na Obado.
Jaji Cecilia Githua anayesikiza kesi ya mauaji dhidi ya Obado, Oyamo na Casper Obiero alifahamishwa Sharon na mwanahabari anayetambuliwa kwa herufi XYZ waliabiri gari muundo wa Toyota Wish nje ya Hoteli Gracia iliyoko kaunti ya Homa-Bay mnamo Septemba 3,2018.
Oyamo anayedaiwa ndiye aliitisha gari hilo la Taxi kuwachukua Sharon na XYZ kuwapeleka kwa Obado alikana kabisa kuwaitishia gari hilo.
Akijitetea kwa siku ya pili mfululizo, Oyamo alisema aliachwa nyuma ndani ya hoteli na alipotoka aliwaona Sharon na XYZ wakiingia taxi hiyo.
“Sikujua waliokuwa ndani ya gari hilo yenye rangi nyeusi. Sikuingia ndani. Niliachwa nje hata nikasaidiwa kupata Boda Boda na mlinzi wa langoni katika hoteli hiyo ya Gracia,” Oyamo alimweleza Jaji Githua.
Msaidizi huyo wa zamani wa Obado alisema alifululiza hadi Migori kwa Boda Boda kujiandaa kwa ziara ya Obado kwenda nchini Rwanda kwa kongamano ya Magavana.
“Nilienda nyumbani kujiandaa kusafiri hadi Rwanda pamoja na Obado. Keshoye Septemba 4,2018 nilipokea simu nyingi zikidai nilimsaliti Sharon na XYZ na kuwakabidhi kwa watekaji nyara ambao wamemuua Sharon. XYZ aliruka kwa gari hilo ka watekaji nyara na kutokomea msituni,” Oyamo alimweleza jaji Githua.
Msaidizi huyo wa Obado aliendelea kusema alirudi Migori baada ya kuamriwa na idara ya mawasiliano gatuzi la Migori ajisalamishe kwa polisi.
“Nilikuwa nimefika Kisiii nikielekea Nairobi Septemba 4,2018 nilipopokea simu ikinitaka nirudi Migori nijisalamishe kwa Polisi,” Oyamo alisema.
Mshtakiwa huyo alieleza mahakama alirudi Migori na kupitia katika makazi rasmi ya Gavana Obado na kurudisha pesa za marupurupu ya safari ya Rwanda na stakabadhi nyingine.
Alimpigia nduguye simu na kumkabidhi pasipoti yake na pesa kisha akajisalamisha kwa polisi waliomhoji kuhusu Sharon na XYZ na kile alichojua kuhusu mauaji ya mwanafunzi.
Oyamo alieleza polisi kwamba alikutana na Sharon na XYZ na kumkabidhi Sharon Sh100,000 alizokuwa amepewa na Obado za kujikimu kwa vile alikuwa na uja uzito wake.
Oyamo alikana alihusika katika mipango ya kumuua Sharon.
Jaji Githua anaendelea kupokea ushahidi kutoka kwa Oyamo ambaye atahojiwa vikali na viongozi wa mashtaka Gikui Gichuhi, Mercy Njoroge na Millicent Kigura.
Bi Gikui alieleza mahakama kwamba ushahidi uliopo ni kwamba Oyamo alihusika katika kupanga mauaji ya Sharon.
Kesi itaendelea Mei 23,2025.