• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
TAHARIRI: Pia tuangalie faida za kongamano hili

TAHARIRI: Pia tuangalie faida za kongamano hili

NA MHARIRI

KONGAMANO kubwa la kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD25) linang’oa nanga Jumanne jijini Nairobi huku likikumbwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini nchini.

Waandalizi wa kongamano hilo – Serikali za Kenya na Denmark pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Uzazi (UNFPA), wametangaza kuwa na malengo makuu matano ya kuangaziwa kati ya leo na Alhamisi.

Miaka 25 iliyopita, mataifa 179 yalikutana jijini Cairo, Misri na kuweka azimio la kuwawezesha wanawake na wasichana, kwa lengo la kuimarisha familia, jamii na mataifa.

Malengo ya kongamano la (ICPD25) ni; haki za afya ya uzazi, kumaliza dhuluma za kijinsia na tabia nyingine zinazowaathiri wanawake, na kuwapa haki ya tiba watu wanaochukuliwa kuwa kinyaa kwa jamii.

Kongamano hili pia linalenga kuvutia mataifa kuunga juhudi hizi kisiasa na kifedha, ili ulimwengu wetu uwe mahali ambapo kila mtu atakuwa na haki ya kutibiwa anapohitaji tiba.

Viongozi wa makanisa na Waislamu wamejitokeza kukashifu kongamano hili, wakisisitiza kuwa lengo pekee ni kuhalalisha uavyaji mimba na ushoga na usagaji.

Wanaamini wanaoendeleza mapenzi ya mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke, hawafai kusamehewa au kuchukuliwa kuwa binadamu.

Wasiwasi huo unaeleweka, ikizingatiwa kuwa Kenya ni taifa ambalo zaidi ya asilimia 99 ni watu wanaoabudu Mwenyezi Mungu.

Lakini nchi yetu inatambua sheria za dini na Katiba yetu. Katika dini zote, mtu hahukumiwi kabla hajasikizwa.

Kifungu cha 33 cha katiba yetu kinatambua haki ya kila mtu kujieleza au kutoa maoni yake. Kwa sasa, viongozi wa kidini na wengine wote walio na pingamizi, wanapaswa kusikiza yatakayosemwa na kisha watapata nafasi ya kukosoa.Si malengo yote ya kongamano hili yenye madhara kwetu.

Kwa mfano kusema kuwa tunahitaji kutilia mkazo kukomesha visa vya vurugu katika ndoa au familia, si vibaya.

Au kwamba mtu anapohitaji matibabu ya dharura yanayohusiana na uzazi, atibiwe kwanza ndipo watu waulize kama yeye ni wa aina hii au ile.

Maishani kila jambo lina uzuri na ubaya wake. Cha muhimu ni watu kusikiza na kuelewa yanayosemwa. Kupitia maelezo yatakayotolewa, ndipo wanaopinga wanaweza kuchukua msimamo imara.

You can share this post!

WASONGA: Fujo za Kibra ni aibu kwa ODM na viongozi wake

HAWASHIKIKI! Manchester City kama vile wameanza kukata tamaa

adminleo