Afya na JamiiMakala

Afueni majaribio ya dawa za wanaume kupanga uzazi yakifanikiwa kwa panya na nyani  

Na MARY WANGARI April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NDOTO ya muda mrefu ya wanandoa kugawana majukumu ya kupanga uzazi huenda ikatimia hivi karibuni, kutokana na uvumbuzi wa kidonge kipya cha wanaume kupanga uzazi ambacho kwa sasa kinapitia majaribio.

Dawa hiyo, inayojulikana kama YCT-529, ni kidonge pekee cha kupanga uzazi kwa wanaume kisicho cha homoni, na pia ndio dawa ya pekee ya aina hiyo inayojaribiwa kwa binadamu kwa sasa.

Wanasayansi wana matumaini kuwa dawa hii itapatikana kwa matumizi ya kawaida kabla ya kumalizika kwa mwongo huu, iwapo itapitishwa na mamlaka za afya.

Kulingana na majaribio ya awali yaliyofanywa kwa panya (mnyama), YCT-529 ina ufanisi wa asilimia 99 katika kuzuia ujauzito, kiwango sawa kabisa na kile cha kupanga uzazi kwa wanawake.

Utafiti huu unaongozwa na timu ya watafiti kutoka taasisi ya YourChoice Therapeutics mjini San Francisco, Chuo Kikuu cha Columbia kilichoko New York, na Chuo cha Dawa cha Chuo Kikuu cha Minnesota.

Kulingana na wataalamu, dawa hii isiyo ya homoni haipunguzi hamu ya ngono kwa wanaume kwa sababu huzuia uzalishaji wa shahawa kwa kuzuia upatikanaji wa Vitamini A kwenye korodani bila kuathiri viwango vya homoni ya testosterone.

Awamu ya kwanza ya utafiti huu iliyohusisha binadamu tayari imekamilika, na wanasayansi wamebaini kuwa dawa hii ni salama kwa matumizi ya wanaume.

Matokeo ya ufanisi na usalama wake yanatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwaka huu, 2025.

Awamu ya pili ya majaribio ya kibinadamu inaendelea New Zealand, ikihusisha kundi dogo la wanaume waliojitolea, na kwa mujibu wa watafiti, mchakato unaendelea vizuri.

Katika awamu ya kwanza ya utafiti iliyochapishwa kwenye Journal of Communication Medicine, wanasayansi walijaribu dawa hiyo kwa panya na nyani.

Baada ya kutumia dawa hiyo kwa muda wa wiki nne, ufanisi wa kuzuia ujauzito ulikuwa asilimia 99 na pia ilisababisha utasa wa muda kwa panya wa kiume.

Kwa nyani, matokeo yalionyesha kuwa idadi ya mbegu ilipungua ndani ya wiki mbili baada ya kuanza kutumia dawa hiyo.

Walipopunguza matumizi ya dawa hiyo, uwezo wa kupata watoto ulirejea kwa panya na nyani, na hakukuwa na athari yoyote ya kiafya iliyoonekana, jambo ambalo lilikuwa muhimu zaidi kwa watafiti.

Kwa nyani, idadi ya mbegu ilirejea kikamilifu kati ya wiki 10 hadi 15, ilhali kwa panya ilichukua wiki sita kurejea katika hali ya kawaida.

“Mfumo salama na wa ufanisi wa mpango wa uzazi kwa wanaume utapanua chaguo la kupanga uzazi kwa wanandoa,” asema mtaalamu wa dawa kutoka Chuo Kikuu cha Minnesota, Gunda Georg.

Iwapo YCT-529 itapitishwa kwa matumizi ya kibiashara, wanaume hatimaye watakuwa na kidonge cha kupanga uzazi cha kutumia kwa mdomo, sawa na kile kilichopatikana kwa wanawake tangu miaka ya 1960.

Inakadiriwa kuwa karibu robo ya wanawake wanaotumia mpango wa uzazi hutumia vidonge vya kupanga uzazi, lakini hadi sasa wanasayansi hawajafanikiwa kubuni njia zinazofanana kwa wanaume.

Kwa sasa, wanaume wana chaguo chache sana za kupanga uzazi: upasuaji wa kuziba mirija ya mbegu, kondomu, na kujitoa kabla ya mshusho (ejaculation).

Kati ya hizo, kondomu na kujitoa kabla ya mshusho ndizo njia pekee zinazoweza kurejeshwa.

Wanawake wana chaguo nyingi za kupanga uzazi. Zipo njia za muda mfupi kama vile vidonge na vipandikizi ambazo zina ufanisi wa takriban asilimia 93.

Kuna pia njia za muda mrefu kama vifaa vya kuingizwa kwenye mfuko wa uzazi (IUD) na vipandikizi vya homoni vinavyokandamiza utoaji wa mayai, ambazo zina ufanisi wa zaidi ya asilimia 99.